• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Azimio la Umoja kumeza Jubilee, ODM

Azimio la Umoja kumeza Jubilee, ODM

Na LEONARD ONYANGO

VYAMA vya ODM na Jubilee vinatarajiwa kumezwa na muungano wa Azimio la Umoja wake Bw Raila Odinga, imebainika.

Hii ilikuwa baada ya Bw Odinga pamoja na washauri wake kugundua kwamba itakuwa vigumu kwa chama cha ODM na Jubilee kupenya katika eneo la Mlima Kenya.Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Amos Kimunya, anatarajiwa kuwasilisha bungeni pendekezo la kufanyia mabadiliko Sheria ya Uchaguzi kuwezesha wanasiasa kuwania viti kwa kutumia tiketi ya muungano au chama.

Hiyo inamaanisha kwamba, chama cha Jubilee huenda kisisimamishe wawaniaji katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, baada ya ushawishi wake wa kisiasa kufifia.Chama cha ODM pia huenda kikasimamisha wawaniaji katika eneo la Nyanza tu na sehemu nyingine za nchi watatoa tiketi za muungano wa Azimio la Umoja endapo mabadiliko hayo ya Bw Kimunya yataidhinishwa na Bunge.

Wabunge ambao sasa wako likizoni, watarejea Bungeni kwa ajili ya vikao maalumu Desemba 21 na Desemba 22, mwaka huu, kujadili miswada mbalimbali inayohusiana na uchaguzi.Mswada wa kufanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi na Mswada wa marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Fedha za Kampeni, ni miongoni mwa miswada itakayojadiliwa.

Mswada wa kufanyia marekebisho Sheria ya Uchaguzi unalenga kuhakikisha kuwa watu wanaoteuliwa kuwa madiwani maalumu ni sharti wawe wamejisajili kuwa wapigakura katika kaunti husika.“Ni wakati wa kujadili miswada hiyo ambapo Bw Kimunya atawasilisha pendekezo la kutaka wanasiasa waruhusiwe kuwania kwa kutumia tiketi ya muungano au chama,” akasema mbunge wa ODM ambaye alitaka jina lake libanwe kwa kuhofia kusutwa na wakuu wake.

Wandani wa Bw Odinga tayari wamewasilisha ombi lao kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu, wakitaka vuguvugu la Azimio la Umoja lisajiliwe kuwa muungano wa kisiasa.Wandani wa Rais Kenyatta kutoka eneo la Mlima Kenya, wamekuwa wakigura Jubilee na kujiunga na vyama vidogo huku wakidai kuwa chama hicho tawala kimepoteza ushawishi wa kisiasa katika ukanda huo.

Magavana James Nyoro (Kiambu), Francis Kimemia (Nyandarua) Lee Kinyanjui (Nakuru) na Ndiritu Muriithi (Laikipia) – ambao ni wandani wa Rais Kenyatta – wametangaza nia yao ya kugura Jubilee.Gavana Kinyanjui tayari amebuni chama chake cha Ubuntu Peoples Forum (UPF) huku kukiwa na tetesi kwamba magavana wengine watatu wanapanga kujiunga na Party of National Unity (PNU) kinachoongozwa na waziri wa Kilimo Peter Munya.Chama cha PNU mwezi uliopita kilitia saini mkataba wa kuunda muungano na ODM.

Magavana hao ambao ni washirika wa karibu wa Bw Odinga walisema wanalenga kuunda muungano ambao utaleta pamoja watu wenye maono sawa nchini. “Tutaungana na Wakenya wenye maono sawa katika eneo la Mlima Kenya na kote nchini.

Muungano huo utakuwa mkubwa kiasi kwamba utabuni serikali ijayo,” akasema Dkt Nyoro.Kiongozi huyo wa ODM anasema kuwa wanaendelea na mazungumzo ya kubuni muungano wa kisiasa na Bw Odinga.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Raia wapewe mafunzo ya kukabili mikasa...

Sababu za Rais ‘kuhepa’ mkutano wa Raila- Wadadisi

T L