• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Baiskeli zaendelea kutumika Nakuru licha ya kupandishwa hadhi kuwa Jiji

Baiskeli zaendelea kutumika Nakuru licha ya kupandishwa hadhi kuwa Jiji

NA MERCY KOSKEI

BAISKELI zinaendelea kutumika kutoa huduma za usafiri na uchukuzi wa umma Nakuru licha ya kupandishwa hadhi kuwa jiji miaka miwili iliyopita na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Baiskeli, hata hivyo, zinatumika katika usafiri wa masafa mafupi Jijini Nakuru.

Novemba 30, 2021 Rais Kenyatta alitunuku Nakuru hati ya jiji, hatua iliyoifanya kuwa jiji la nne nchini baada ya Kisumu, Mombasa na Nairobi.

Licha ya kupandishwa hadhi, katika ziara yako Jijini Nakuru utakutana na baiskeli zimeegeshwa maeneo tofauti zikisubiri wateja.

Taifa Leo Digitali ilikutana na Bw Benson Otieno, 40, mhudumu katika egesho lake katika barabara ya Sport Club akisubiri kuona ikiwa atabahatika kupata mteja.

Otieno hufika kazini saa mbili asubuhi hadi saa mbili usiku, na kwa siku huunda Sh500.

Bw Otieno anafichua kwamba amekuwa katika biashara ya huduma za baiskeli kwa muda wa miaka minne sasa, baada ya kumwaga unga katika kampuni aliyokuwa akifanyia kazi.

Anasema kuwa kwa kutumia akiba yake ya Sh9, 000 alinunua baiskeli akiwa na matuamini ya kukimu familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi, hatua ambayo anasema hajawahi kujutia tangu kujitosa katika biashara hiyo 2019.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Otieno alisema licha ya pikipiki kuwa maarufu kutokana na kasi yake ikilinganishwa na baiskeli, wengi wanapendelea kuzitumia kwa sababu ya usalama wake na bei nafuu.

“Kazi hii ndiyo jembe langu kulimia familia…Wengi wanapendelea baiskeli kwa sababu ya bei yake nafuu. Kwa muda ambao nimefanya kazi hii imenisaidia sana,” alisimulia mhudumu huyo wa baiskeli.

Mita mia tano hivi kutoka kwa Otieno, tunakutana na Bw Zacharia Mutua, ambaye pia amekuwa katika sekta hii kwa miaka mitatu sasa.

Zacharia Mutua, mhudumu wa baiskeli – bodaboda Jijini Nakuru. PICHA|MERCY KOSKEI

Anasema alilazimika kujitosa katika biashara ya bodaboda baada ya wezi kuvamia duka lake na kumlazimu kutafuta njia mbadala kukithi familia yake riziki.

Alidokeza, kwa bahati nzuri rafiki yake alimpa baiskeli angaa kusukuma gurudumu la maisha.

Alikuwa akilipa Sh100 kwa siku, na mwaka mmoja baadaye alifanikiwa kununua baiskeli yake mwenyewe.

Bw Mutua anasema kuwa kwa sasa anatunza familia yake, ikiwa ni pamoja na kulipa karo ya shule, licha ya wengi kudharau na kudumisha kazi ya huduma za bodaboda kwa kutumia baiskeli.

“Ushindani uko juu kati yetu. Lakini kila mtu ana wateja wake. Uhusiano wetu na waendesha pikipiki ni mzuri. Sote hatuwezi kuingia katika biashara ya pikipiki. Tunaheshimiana,” alielezea.

Taswira ya Nakuru baiskeli kutumika katika usafiri na uchukuzi, ni kinyume na miji mingine kama vile Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Demu anadai pesa ili anipe asali, huyo ni mpenzi aina gani?

Wamuchomba asimulia alivyochapwa na babake kwa kutokea...

T L