• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
BALLON D’OR: Messi tena? Lewandowski kachezwa!

BALLON D’OR: Messi tena? Lewandowski kachezwa!

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

SUPASTAA Lionel Messi alinyakua tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2021 baada ya kubwaga wapinzani wake wakuu Robert Lewandowski na Jorge Luiz Frello Filho almaarufu Jorginho, mnamo Jumatatu usiku.

Hata hivyo, mchana-nyavu matata Lewandowski alikuwa amepigiwa upatu mkubwa kutwaa tuzo hiyo, inayopewa mwanasoka bora wa mwaka.

Baadhi ya wafuasi wa soka walisikitikia uamuzi wa kutochaguliwa kwa Lewandowski kama mwanasoka bora.

Mshindi mara tano Cristiano Ronaldo alimaliza nambari sita, ya chini kabisa tangu 2010.

Gazeti la Bild kutoka Ujerumani lilisema Robert Lewandowski “aliibiwa” kwa kuorodheshwa wa pili, ambayo hiyo ni “sakata”.

Tovuti ya talkSPORT ilimuonea huruma straika huyo matata wa Bayern Munich ya Ujerumani.

“Sidhani ana ufuasi mkubwa duniani. Hasisimui wapigakura. Sidhani kama Messi alistahili tuzo hiyo. Lewandowski ndiye alifaa kuwa mshindi,” ilisema.

Jumla ya wanahabari 180 kutoka kote duniani ndio hupiga kura hiyo.

Ilitilia shaka wenyeji wa tuzo hiyo France Football kuanzisha kitengo kipya cha mfumaji matata ili kumpa Lewandowski kitulizo.

“Itakuwaje Lewandowski ni mfungaji hodari wa mabao, lakini nambari mbili kwenye tuzo ya Ballon d’Or?” tovuti hiyo iliuliza.

Messi sasa ni mshindi wa Ballon d’Or mara saba – 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021.

Lewandowski wa Bayern ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) aliambulia alama 580.

Kiungo mkabaji Jorginho, ambaye aliongoza Chelsea kutawala Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na pia Italia kuibuka mabingwa wa Kombe la Euro 2020, aliridhika na nafasi ya tatu kwa pointi 460.

Naye mshambuliaji matata wa Liverpool, Mohamed Salah – ambaye timu yake itapepetana na Everton ligini uga wa Goodison Park leo Jumatano usiku – alikuwa nambari saba.

Kipa wa Italia na Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, alitawazwa kipa bora.

Hii ni licha ya takwimu za kipa wa Senegal na Chelsea, Edouard Mendy, kuwa nzuri zaidi.

You can share this post!

MOHAMED OSMAN: Mapendekezo ya Glagsow kuhusu mabadiliko ya...

Kenya kusaka leo tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

T L