• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Baraza la Magavana Nchini lamruka Gachagua kuhusu mgano wa fedha za El Nino

Baraza la Magavana Nchini lamruka Gachagua kuhusu mgano wa fedha za El Nino

WINNIE ATIENO NA JURGEN NAMBEKA

BARAZA la magavana (CoG) limevunja kimya chake kuhusu mvutano ambao umekuwa ukishuhudiwa baina ya gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusiana na kutolewa kwa fedha za kukabiliana na mvua za El-Nino.

Katika barua iliyotazamwa na Taifa Leo Dijitali baraza hilo kupitia kwa mwenyekiti wake, Bi Anne Waiguru, lilikanusha madai ya kupokea fedha za kukabiliana na mvua hizo.

“Hadi tarehe ya leo (Jumatano, Novemba 22, 2023, tungependa kueleza kuwa serikali za kaunti hazijapokea fedha zozote kutoka kwa hazina ya kitaifa zilizotengwa kushughulikia mvua nyingi inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini,” ikasema sehemu ya barua hiyo.

Baraza hilo lilieleza kuwa serikali za kaunti zilikuwa zikisubiri mgao wa hadi Sh62.58 bilioni ambao hupeanwa kwa kila kaunti kila mwezi.

Baraza hilo lilikashifu semi zinazotolewa kuashiria kuwa serikali za kaunti zilikuwa zimepewa mgao kukabiliana na El Nino, na athari zake.

“Tunataka kueleza kuwa semi hizo zinakiuka umoja na ushirikiano wa serikali za kaunti na ya kitaifa kama ilivyo kwenye Kipengee cha Sita sehemu ya Pili ya Katiba,” ikasema barua hiyo.

Haya yanajiri magavana wa upinzani wakipinga semi za Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kwamba wamepokea fedha za kukabiliana na athari za mafuriko.

Wakiongozwa na Bw Abdulswamad Nassir (Mombasa) na mwenzake James Orengo (Siaya), magavana hao wamemtaja Bw Gachagua kuwa mwongo.

“Ukweli ni kwamba, serikali kuu mpaka wa leo hawajatoa hata senti moja kwa serikali za kaunti zote nchini. Hata kule kwake Nyeri, hawajatoa hata ndururu. Hata kule Siaya tumekabiliwa na mafuriko, watu wamehama na wahanga wana matatizo ya makazi na chakula,” alisema Bw Orengo.

Gavana Orengo na Bw Nassir waliitaka serikali kuu kueleza bayana fedha zilizotengwa kukabiliana na El Nino zilikopelekwa.

Alisema serikali ya Kenya Kwanza ni ya unafiki na imekumbwa na shutma za ufisadi.

“Naibu wa Rais ni muongo, kila anachoongea ni uongo mtupu. Ahadi anazotoa hatimizi. Watu waache utapeli,” aliongeza Bw Orengo.

Aliwasihi wakazi wa Mombasa kusimama kidete na ODM ili chama hicho cha upinzani kiendelee kupata uungwaji mkono mkubwa.

Naye Bw Nassir alisema ataendelea kuwa mwanachama wa ODM akisisitiza kuwa kinara wa upinzani Bw Raila Odinga amemlea kisiasa.

Alimtaka Bw Gachagua kuwa mkweli.

“Waswahili wanamsemo, ‘Ukweli hauna haja ya nguzo ya kusimama. Hakuna hata ndururu imefika Mombasa’,” alisema Bw Orengo.

Naibu wa Rais akihutubu eneo la Karen, Jijini Nairobi, alieleza kuwa magavana hawapaswi kusubiri fedha zozote kutoka kwa serikali kuu.

“Nimesikia magavana wakisema hawajapokea fedha za El Nino, hakuna fedha kama hizo zinazokuja. Tunawataka watumie fedha za dharura au wabadilishe mkondo wa fedha zingine,” akasema Bw Gachagua.

Gavana Nassir alisema serikali za kaunti zimekuwa zikishirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kusaidia wahanga wa El Nino.

“Mimi hata naomba Mungu tupewe hizo fedha. Usidanganye watu wakati wanapitia dhiki, usidhulumu watu,” alisema Bw Nassir.

 

  • Tags

You can share this post!

Vuguvugu la Bunge la Mwananchi lataka leseni ya kampuni ya...

Gachagua ataka DCI itenge nafasi za kazi kwa wasomi,...

T L