• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Bendi ya Qlassic inavyojizolea umaarufu jijini Nairobi

Bendi ya Qlassic inavyojizolea umaarufu jijini Nairobi

Na MAGDALENE WANJA

ILIANZA shughuli zake kama mojawapo ya njia za kupitisha wakati baina na miongoni mwa marafiki waliokuwa wakifanya kazi katika bendi mbalimbali.

Wakati mwingi walikutana mwishoni mwa wiki na kila walipokuwa wakiimba, walihisi kuwa walifanya vyema zaidi kushinda kazi zao za kawaida.

Ni hapo ndipo walipofikia uamuzi wa kuja pamoja ili kuunda bendi ambayo ingewasaidia kutimiza ndoto zao.

Bendi ya Qlassic ilianzishwa mwaka mmoja uliopita na umaarufu wake unaendelea kusikika jijini Nairobi na sehemu zilizoko karibu.

Hi ni kulingana na Bi Maria Ngoma ambaye ni mwimbaji – lead vocalist – katika bendi hiyo.

“Uimbaji wetu hukupa nafasi ya kufurahia nyimbo za aina mbalimbali katika kikao kimoja,” anasema Bi Ngoma.

Bendi hiyo ya Qlassic iko chini ya usimamizi wa kampuni ya Top Notch Entertainment ambayo ina bendi mbili.

“Kuna bendi mbili chini ya usimamizi wa kampuni hiyo na kila moja ina msichana mmoja kama lead vocalist. Kuwa mwanamke wa kipekee katika bendi kunafanya msanii kuhisi wa maana lakini pia akifahamu kuna majukumu yake,” akasema.

Bendi hiyo kufikia sasa imetunga nyimbo tano ambazo bado kurekodiwa.

“Kando na kutupa nafasi ya kuwasiliana kupitia nyimbo, bendi hii pia ni nafasi ya kazi ambayo imetuwezesha kulisha familia zetu,” akasema Bi Ngoma.

Bendi hiyo ina watu wa umri mdogo hivyo kufanya iwe rahisi kushika nyimbo mbalimbali kwa urahisi.

“Tunaweza kufanya nyimbo mbalimbali bila ugumu wowote na kujifunza huchukua muda mfupi,” akaongeza.

Hata hivyo, wamekutwa na baadhi ya changamoto ikiwemo malipo duni kutoka kwa baadhi ya wateja.

“Mtindo wa Live band ndio unapata umaarufu nchini Kenya na baadhi ya watu hawataki kulipia huduma hiyo kama inavyostahili,” akasema Bi Ngoma akirejelea utumbuizaji mubashara.

Wengine katika bendi hiyo ni pamoja na Jonathan Msolo (lead guitarist), Dan Saxo (saxophonist), Owitti Bassman (bass player),Bonny Lwanga (keyboard player), David Fernado (drummer) na Jay Madini (vocalist).

You can share this post!

Sonko afika kuhojiwa makao makuu ya EACC

Wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Mumias watimuliwa

adminleo