• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Binadamu ndio wabaya!

Binadamu ndio wabaya!

HAKIKA hii dunia si mbaya, binadamu ndio wabaya. Hivi yule aliyeanzisha ule uvumi kuwa DJ Evolve kafa wakati mwenzenu yupo hai, alikuwa akiwaza nini?

Hivi ni kwa nini baadhi yetu tupo hivi? Ni kwa nini tunakosa utu? Ni dhahiri shahiri kuwa kila nafsi lazima itaonja mauti siku moja ila ni kwa nini umzushie mtu aliye hai kifo? Kwa faida gani lakini? Jumanne wiki hii, DJ Evolve ndiye aliyekuwa akitrendi kwenye Twitter madai yakiwa ni kwamba jamaa kauma pamba.

Pengine kwa yule asiyekuwa na picha ya ninayemzungumzia, basi acha nikufahamishe. Unamkumbuka yule DJ aliyepigwa risasi na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino mwaka jana? Ni stori iliyoangaziwa kwa wiki kadhaa kiasi cha kumpelekea Mhesh kukimbia mahakamani kuomba vyombo vya habari vizuiliwe kuangazia stori hiyo.

DJ Evolve alikuwa akifanya kazi yake ya U-deejay katika klabu ya B-Club iliyopo mtaa wa Kilimani. Ni moja ya kumbi za burudani anazozihusudu sana Babu Owino. Wawili hawa walikuwa wamefahamiana kwa muda ila siku moja DJ Evolve alitofautiana naye kwenye klabu hiyo na mbunge huyo akaishia kumlipua na marisasi.

Risasi iliyopenyeza kwenye shingo yake ndio ilimwacha hoi.Toka wakati huo kawa kilema. Hawezi kutembea kama zamani, analishwa kwa mirija. Maisha yake siku hizi yapo kitandani tu. Babu Owino alishurutishwa na mahakama kusimamia matibabu yake.

Alitumia zaidi ya Sh16 milioni kwenye matibabu yake.DJ Evolve ana zaidi ya nusu mwaka toka aliporuhusiwa kuondoka hospitalini kwenda nyumbani. Bado tu hayupo sawa. Hawezi kutembea na hata kwenda haja ni lazima asaidiwe. Kwa ufupi hayupo kama zamani hata baada ya kutoka hospitalini.

Huyu ndiye mtu aliyezushiwa kifo.Napata taabu sana kumwelewa aliyeanzisha uvumi huo. Wakati mwenzio anajitahidi kupambana kuishi na hata ikiwezekana arejee katika hali yake ya zamani, yupo mtu mbinafsi aliyeshikwa na mawazo ya kumzushia kifo. Kwa nini lakini? Kwa faida gani?Ndio mwanzo ameanza kuwa na uwezo wa kuketi.

Babake akipinga uzushi huo alisema mwanawe ameanza kuonyesha dalili za afya yake kuboreka kwani siku hizi ana uwezo wa kuketi kwa lisaa. Haikuwa hivyo toka majanga haya yalipompata. Aliyeanzisha uvumi huo alikuwa na uhakika kuwa stori ingetrendi.Machungu aliyopitia DJ Evolve hakika yeye kuponea kifo ni muujiza.

Ndio sababu huyu nongwe alijua kabisa stori yake itauza. Sijui ni kwa nini Wakenya sisi hukosa utu. Kuna vitu vya kufanyia dhihaka ila wakati mwingine tunavuka mipaka kama hili la DJ Evolve. Hivi ingelikuwa ni wewe unazushiwa kifo, ungejihisi vipi? Wakati mwingine tuwe na busara za kuwaza kabla ya kutamka au kuandika hasa mitandaoni.

Inasikitisha sana kuwa tumefikia huku. Haya machungu sijui tunayatoa wapi. Kila kukicha lazima kuwepo na jambo hasi linalotrendi. Muda mwingi huwa natamani kuona jema likitrendi huku Kenya lakini wapi. Najua kila binadamu ana hulka na tabia yake binafsi, ila naomba dua sana Allah atujaliye busara ya kuwa watu waelewa kuliko tulivyo.

  • Tags

You can share this post!

Teuzi zote zifanywe kwa kuzingatia katiba bila ubaguzi

Adai kufungiwa boma hadi abaini ukweli wa kifo cha mtoto...