• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Boko Haram waua 23, 15 waangamizwa Burkina Faso

Boko Haram waua 23, 15 waangamizwa Burkina Faso

NA MASHIRIKA

WANAMGAMBO wa Boko Haram Jumamosi, walivamia waombolezaji katika jimbo la Borno lililoko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na kuua watu 23 ambao walikuwa wamehudhuria matanga.

Wapiganaji hao wanaripotiwa kufika saa nne na nusu usiku wakiwa katika pikipiki tatu na wakaanza kufyatua risasi dhidi ya waombolezaji, katika wilaya ya Nganzai, iliyoko hatua chache kutoka jiji la Maiduguri.

Wakazi na walinda usalama wa eneo hilo walisema waliovamiwa walikuwa wakitoka kijiji cha Goni Abachari, kuelekea kijiji cha Badu Kuluwiu. Walikuwa wameenda kuhudhuria maombolezi ya mtu wa familia yao.

“Walinda usalama wetu walipata miili 23 katika eneo hilo lililovamiwa,” akasema Bunu Bakar, kiongozi wa walinda usalama eneo hilo.

Miili ya waliokufa ilichukuliwa baada ya walioponea kuenda kijijini na kufahamishana kuhusu uvamizi huo.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa wapiganaji wa Boko Haram kuvamia wilaya hiyo ya Nganzai, kwani Septemba mwaka jana waliua watu wanane, ambao walijaribu kuwazuia kuiba mifugo yao, katika vijiji viwili eneo hilo.

Alhamisi, wapiganaji wa Boko Haram walivamia kambi ya wakimbizi nje ya Maiduguri, ambapo waliua wakazi wawili na wakaiba vyakula, baada ya kuchoma kambi ya kijeshi.

Uvamizi kutoka kundi hilo haramu umedumu kwa takriban miaka kumi, ukisambaa katika mataifa jirani kama Chad, Niger na Cameroon, ambapo zaidi ya watu 27,000 wamepoteza maisha, na zaidi ya milioni mbili kuhama makwao.

Wakati huo huo, watu wenye silaha walivamia kijiji kimoja Burkina Faso na wakawaua watu 15, wakateketeza maduka na pikipiki.

Iliripotiwa kuwa zaidi ya watu 20 walihusika katika uvamizi huo wa kijiji cha Diblou, Gavana wa jimbo hilo la Sahel Casimir Segueda akisema kituo cha kibiashara kiliteketezwa.

Jimbo hilo limekuwa likikumbwa na uvamizi wa kigaidi kwa takriban miaka minne, ukisambaa kutoka kaskazini ambapo ulianzia hadi mashariki katika mpaka wa Togo na Benin.

Uvamizi mwingi umekuwa ukihusishwa na kundi haramu la Ansarul Isalm, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mali, Desemba 2016.

Kundi la JNIM ambalo lilikiri kuunga mkono kundi haramu la Al-Qaeda pia limekuwa likilaumiwa kwa uvamizi.

Makundi hayo yanadaiwa kuwa ndiyo yamesababisha jumla ya vifo vya watu 500 tangu 2015, jiji kuu la Ouagadougou likiwa limevamiwa mara tatu.

You can share this post!

Viongozi wa Magharibi wamlilia Rais awape waziri serikalini

Jombi azimia kung’amua mke ana mwanaharamu

adminleo