• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Brescia wajuta kumsajili Mario Balotelli

Brescia wajuta kumsajili Mario Balotelli

Na CHRIS ADUNGO

MMILIKI wa kikosi cha Brescia kinachoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Massimo Cellino, amesema kwamba anajutia sana hatua ya kuwahi kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Manchester City na Liverpool, Mario Balotelli.

Tangu aingie katika sajili rasmi ya Brescia mwanzoni mwa msimu huu, Balotelli, 29, ambaye ni mzawa wa Italia, amefunga jumla ya mabao matano akiwa mchezaji wa kikosi hicho.

Hata hivyo, Cellino amesema kwamba Balotelli kwa sasa yuko huru kuondoka kambini mwa Brescia ambao wananing’inia pembamba mkiani mwa jedwali la Serie A kwa alama 16 kutokana na jumla ya michuano 26 iliyopita.

“Balotelli amekuwa akikosa vipindi vya mazoezi, hawajibikii kikosi kwa kujituma ipasavyo na hana maazimio yoyote yanayohusiana na maendeleo ya klabu. Hilo ndilo tatizo kubwa alilonalo,” akasema Cellino.

“Balotelli alitia saini mkataba akiwa mchezaji wa Serie A. Hana mkataba na kikosi chochote cha Serie B. Kwa hivyo, iwapo Brescia watashushushwa ngazi kwenye Serie A msimu huu, sidhani atakuwa na sababu yoyote ya kuendelea kuvalia jezi zetu tukiwa katika Ligi ya Daraja ya Kwanza (Serie B).

“Nadhani sisi sote tulikosea katika kumsajili. Nilidhani ujio wake Brescia, ambako ni mji alikozaliwa, ungemfanya ajitume zaidi. Kumbe mambo yaliwa kinyume. Kwa upande mwingine, nadhani hakuwa katika uhusiano mzuri na kocha wa zamani wa Brescia, Eugenio Corini ambaye hakuelewa kabisa mienendo yake,” akasema Cellino.

Balotell amebaguliwa kwa msingi wa rangi yake mara mbili katika Serie A msimu huu huku Lazio wakitozwa faini ya Sh2.5 milioni kwa kushindwa kuwadhibiti mashabiki wao waliokuwa wakimrushia Balotelli cheche za matusi uwanjani kwa sababu ya rangi yake.

You can share this post!

Kipenga cha kuashiria kurejelewa kwa Serie A kupulizwa...

RIZIKI: Kwa zaidi ya miaka 20 anategemea uchomeleaji wa...

adminleo