• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Wenyeji Cameroon wafungua fainali za AFCON 2021 kwa ushindi dhidi ya Bukina Faso

Wenyeji Cameroon wafungua fainali za AFCON 2021 kwa ushindi dhidi ya Bukina Faso

Na MASHIRIKA

WENYEJI Cameroon walitoka nyuma na kupepeta Burkina Faso 2-1 katika mchuano wa kufungua makala ya 33 ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Jumapili ugani Paul Biya, Yaounde.

Gustavo Sangare aliwaweka Burkina Faso kifua mbele katika dakika ya 24 kabla ya nahodha Vincent Aboubakar kufungia Cameroon penalti mbili za haraka kunako dakika za 40 na 45 mtawalia. Aboubakar anayechezea klabu ya Al Nassr nchini Saudi Arabia ndiye alifunga bao la ushindi na kuongoza Cameroon kuzamisha Misri 2-1 katika fainali ya AFCON 2017 nchini Gabon.

Kipa Andre Onana wa Ajax nchini Uholanzi alifanya kazi ya ziada katikati ya michuma ya Cameroon katika kipindi cha pili na kunyima Burkina Faso nafasi nyingi za wazi za kurejea mchezoni.

Chini ya kocha Toni Conceicao, Cameroon sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi A kwa alama tatu sawa na Cape Verde waliozamisha Ethiopia 1-0 katika mchuano wa pili uliosakatiwa pia uwanjani Paul Biya.

Cameroon wanaoshikilia nafasi ya 50 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), wanawania taji la AFCON kwa mara ya sita huku nambari 60 Burkina Faso waliowahi kutinga fainali ya 2013 wakiwinda ufalme kwa mara ya kwanza katika historia.

Indomitable Lions ya Cameroon ilifuzu kwa fainali za mwaka huu baada ya kujizolea alama 11 kutokana na mechi sita. Baada ya kutamalaki makala ya 2017, Cameroon walidenguliwa na Nigeria katika hatua ya 16-bora mnamo 2019 nchini Misri kwa kichapo cha 3-2.

Mechi ya Jumapili ilikuwa ya kwanza kwa Cameroon kushinda Burkina Faso kutokana na michuano mitano iliyopita. Baada ya kutinga fainali ya AFCON 2013, Burkina Faso walidenguliwa katika hatua ya makundi mnamo 2015, wakaingia nusu-fainali mnamo 2017 na wakashindwa kabisa kufuzu kwa kivumbi cha 2019.

Zaidi ya kujivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi za kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka huu, Burkina Faso walijitosa ulingoni wakiwa na motisha tele baada ya kupepeta Gabon 3-0 kirafiki mnamo Januari 2, 2022.

Licha ya kukosa sehemu kubwa ya kampeni za Cameroon kwa tuhuma za kutumia pufya, kipa Onana alimng’oa mlinda-lango Devis Epassy michumani.

Burkina Faso walitegemea pakubwa maarifa ya Bertrand Traore aliyewafungia bao la pekee na la ushindi dhidi ya Cameroon katika mechi ya kupimana nguvu miaka minne iliyopita. Safu ya mbele ya Cameroon ilijivunia pia huduma za Karl Toko Ekambi (Lyon, Ufaransa) na Eric Maxim Choupo-Moting (Bayern Munich, Ujerumani).

Conceicao amekiri kwamba kikosi chake cha Cameroon kina presha ya kusajili matokeo ya kuridhisha kwenye fainali za AFCON mwaka huu kwa sababu mashabiki “hawatawasamehe wakifeli”.

“Mashabiki wana matarajio makubwa kwa sababu kivumbi hiki kinafanyika nyumbani na kikosi kimejiandaa vya kutosha. Wana kila sababu ya kutarajia makuu kwa sababu ya rekodi nzuri ya Cameroon kwenye fainali za AFCON na Kombe la Dunia,” akasema.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Viongozi wa kidini walaumu Joho kwa kuachia wafanyakazi njaa

Watano waachiliwa kwa madai ya kubomoa ukuta wa kampuni...

T L