• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
CBC: Kuppet pia wana malalamishi

CBC: Kuppet pia wana malalamishi

Na KENYA NEWS AGENCY

CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) kimeitaka Wizara ya Elimu kuhusisha wadau wote katika utekelezaji wa mtaala wa umilisi na utendaji (CBC).

Chama hicho kimesema wazazi na walimu wanakabiliwa na changamoto kuelewa mfumo huo mpya, ambao utekelezaji umefikia hatua ya Gredi 5.

Akiongea na wanahabari mjini Kisii, mwenyekiti wa Kuppet tawi hilo, Bw Laban Bosire Ouko, alisema CBC ni mtaala unaowafaa zaidi wanafunzi katika maeneo ya mijini kuliko mashambani.

Hii ni kwa sababu wanafunzi wa mashambani wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa hitajika kufanya mazoezi wanayopewa.

“Walimu wa shule za upili wanafaa kuwa wameandaliwa kufikia sasa ili kupokea wanafunzi wa kwanza wa CBC miaka michache ijayo. Hilo halijafanyika. Isitoshe, hatujui masomo ambayo yanafaa kufundishwa katika shule za upili za daraja la chini na zile za daraja la juu kwenye mfumo huo,” akasema Bw Ouko.

Kiongozi huyo alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuharakisha mafunzo ya kuwaanda walimu wa upili kabla yao kuwapokea wanafunzi hao wa kwanza.

“Wakati huu ambapo taifa linakabiliwa na changamoto za kila aina katika kuhakikisha mtaala mpya wa CBC unafanikiwa, pia ni muhimu kwa serikali kuhakikisha imeimarisha malipo ya walimu. Hii ni kwa sababu wao ndio kiungo kuu katika ufanisi wa mfumo huo,” aliongeza.

Katibu wa Kuppet tawi la Kisii, Bw Joseph Abincha, alidai kuwa masomo yanayofundishwa katika mtaala huo ni magumu kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.

Aliitaka serikali kuangalia upya masomo hayo kwa lengo la kuyarekebisha na kupunguza.

“Utapata mwanafunzi wa Gredi 4 akifanya zoezi la hisabati ambalo linapaswa kufanywa na mwanafunzi wa kiwango cha shule ya upili,” alisema Bw Abincha.

Afisa mwingine wa Kuppet tawi la Kisii, Bw Omari Otungu, aliunga mkono kauli ya Bw Ouko na kudai kuwa walimu wengi wa shule za msingi hawajaandaliwa ipasavyo kufundisha mtaala wa CBC.

“Pendekezo la wengi ni kwamba tunahitaji kuwaandaa walimu ili watekeleza vyema CBC. Ufanisi wake unahitaji mashauriano na mafunzo kwa walimu wetu,” Bw Otungu alisisitiza.

Naye mkazi wa Kisii Bw Wilber Chweya alisema wazazi wengi hawafahamu vitabu vinavyohitajika katika ufundishaji wa CBC.

You can share this post!

Suarez afunga mabao mawili na kusaidia Atletico Madrid...

Mchoraji vibonzo wa ‘Taifa Leo’ ang’aa