• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
CF Montreal anayochezea Wanyama yang’ata Cincinnati Ligi Kuu ya MLS

CF Montreal anayochezea Wanyama yang’ata Cincinnati Ligi Kuu ya MLS

Na GEOFFREY ANENE

CF Montreal, ambayo imeajiri nyota Victor Wanyama, ilizoa alama tatu muhimu kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) baada ya kuzaba Cincinnati 5-4 katika mechi yake ya kwanza baada ya muda mrefu ugani Saputo jijini Montreal mapema Julai 19.

Kosa la kiungo huyo Mkenya nje ya kisanduku chao alipopokonywa mpira na mshambuliaji Mbrazil Brenner lilitunuku Cincinnati bao la ufunguzi dakika ya sita. Brenner alipasia kiungo wa Argentina, Lucia Acosta mpira ambaye alimegea Haris Medunjanin mpira aliokamilisha kupitia mguu wake wa kushoto.

Kisha, Brenner aliimarisha uongozi wa wageni hao 2-0 dakika ya 14 aliponufaika na kosa la kipa James Pantemis kutoondosha pasi aliyorudishiwa na mchezaji wake ndani ya kisanduku.Wanyama kisha alisuka pasi safi ndani ya kisanduku pembeni kushoto ambayo Lassi Lappalainen alisukuma krosi murwa ndani ya kisanduku iliyokamilishwa na Mason Toye kupitia kwa kichwa dakika ya 21.

Joaquin Torres alisawazisha 2-2 dakika ya 34 baada ya kombora la kwanza la Wanyama kutemwa na kipa Kenneth Vermeer.Gustavo Vallecilla alirejesha Cincinnati kifua mbele 3-2 dakika ya 42 baada ya kukamilisha pasi iliyopatikana beki Rudy Camacho alipojkwaa nje ya kisanduku na kumpa winga Alvaro Barreal nafasi ya kuchanja krosi mbele ya lango.

Brenner alifanya mabao ya Cincinnati kuwa 4-2 mapema katika kipindi cha pili. Hata hivyo, Toye alifungia Montreal bao la tatu dakika ya 72 kupitia penalti baada ya Vermeer kumuangusha ndani ya kisanduku.Ahmed Hamdi alihakikishia Montreal ushindi alipofuma wavuni mabao mawili katika dakika 16 za mwisho.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo wa Montreal ambayo haijapoteza mechi sita zilizopita.Vijana wa kocha Wilfried Nancy wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 22. Wanatofautiana na nambari tatu Orlando City na nambari tano Nashville kwa ubora wa magoli. Wote watatu wamesakata michuano 13 kwenye ligi hiyo ya Ukanda wa Mashariki ya klabu 14.

New England Revolution na Philadelphia zinapatikana katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 27 na 23 baada ya kujibwaga uwanjani mara 14.Seattle Sounders (alama 29), Sporting Kansas City (26), Los Angeles Galaxy (24), Colorado Rapids (21) na Los Angeles FC (21) zinashikilia nafasi tano za kwanza kwa Ukanda wa Magharibi.

Matokeo (Julai 18): Atlanta United 0 New England Revolution 1, Columbus 2 New York City 1, Philadelphia 2 D.C. United 1, Montreal 5 Cincinnati 4, Toronto 1 Orlando City 1, Nashville 5 Chicago 1, Colorado Rapids 1 San Jose Earthquakes 1, Vancouver Whitecaps 2 Los Angeles Galaxy 1, Los Angeles FC 2 Real Salt Lake 1, Portland 1 FC Dallas 0, Minnesota 1 Seattle Sounders 0.

  • Tags

You can share this post!

Mabingwa warejea!

Wezi wa mifugo wauawa Samburu