• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Chama cha ANC chalaumu siasa za Uhuru, Raila kufuatia uchomaji wa afisi zao

Chama cha ANC chalaumu siasa za Uhuru, Raila kufuatia uchomaji wa afisi zao

BENSON AMADALA na VALENTINE OBARA

CHAMA cha Amani National Congress (ANC) kimelaumu wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, kwa kuchochea uchomaji wa afisi ya chama hicho katika Kaunti ya Kakamega.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Barrack Muluka, alisema wanaamini kisa hicho cha usiku wa kuamkia Jumatatu kilisababishwa na watu wanaotaka kuwalazimisha kujiunga na miungano mipya ya kisiasa.

Ingawa hakutaja yeyote, taarifa yake iliashiria kulalamikia juhudi za baadhi ya viongozi wa eneo hilo ambao humtaka kinara wa ANC Musalia Mudavadi pamoja na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula kuweka mkataba wa ushirikiano na Rais Kenyatta jinsi vyama kadhaa vikuu vilivyofanya.

“Hakuna kiwango chochote cha vitisho itatufanya tuangamize siasa ya demokrasia ya vyama vingi. Tunaomba idara ya polisi iharakishe kukamata waliohusika,” akasema kwenye taarifa.

Afisi za ANC zilichomwa na watu wasiojulikana Jumapili usiku.

Moto ulizuka wakati watu hao walipovunja dirisha wakarusha kitu kilichosababisha moto kisha wakatoroka.

Mwenyekiti wa ANC, tawi la Kakamega, Bw Julius Arunga alisema moto uliharibu baadhi ya stakabadhi lakini ukazimwa kabla usambae katika sehemu nyingine.

Afisi hiyo iliyo katika mtaa wa Amalemba huwa haina mlinzi.

Mbunge wa Lurambi, Bw Titus Khamala ambaye alitembelea afisi hizo alikashifu kitendo hicho.

“Tukio hili ni ishara wazi kuwa kuna watu wanaotaka kumdhalilisha kiongozi wa chama chetu na kuvuruga azimio lake la kuwania urais 2022 lakini inafaa wajue hatutalegeza msimamo wetu,” akasema Bw Khamala.

Hivi majuzi, chama hicho kiliamua kumtimua Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala kwa misimamo yake ya kuegemea upande wa Bw Odinga kisiasa licha ya kuwa ni mwanachama wa ANC.

Kamanda wa polisi eneo la Magharibi, Bi Peris Kimani alisema kisa hicho cha moto kinachunguzwa.

“Tumekusanya sampuli za kemikali ambayo ilitumiwa kuanzisha moto huo na wapelelezi wanaendeleza uchunguzi,” akasema Bi Kimani.

  • Tags

You can share this post!

Raha yake kuua wanawake?

Mawakili wa Ngilu wavamiwa bunge la kaunti

adminleo