• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:31 PM
Chapati Festival: Krismasi ya mapema Riruta

Chapati Festival: Krismasi ya mapema Riruta

NA FRIDAH OKACHI

WAPITANJIA katika wadi ya Riruta, eneobunge la Dagoretti Kusini, mnamo Jumamosi walifurahia mlo wa bure ulioandaliwa na kundi la wanawake kuwezesha familia zisizojiweza kusherekea Krismasi.

Mwenyekiti wa kundi hilo la Chapati Festival, Bi Christine Mugo, alisema walikusanya pesa na kununua chakula kulisha mamia ya familia za watu wasioweza kupata chakula msimu huu.

“Siku ya leo tunapika chapati, wali na kitoweo ili watoto wa mitaani na familia ambazo hazina chakula ziweze kunufaika kama wale ambao tayari wana chakula nyumbani,” alisema Bi Mugo.

Mwenyekiti wa Chapati Festival Bi Christine Mugo akiwa amesimama huku akiangalia jinsi ambavyo shughuli hiyo inafanyika. PICHA | FRIDAH OKACHI

Pia, Bi Mugo alisema kujitolea kwa kufanya mapishi hayo, kuliruhusu familia za mapato ya chini zaidi kubeba cha kuwafaa nyumbani.

“Kuna yule hana nafasi ya kuenda mashambani au hana chakala cha kupika kwake. Kwa hivyo, tunakaribisha kila mmoja aje hapa ale,” aliongezea Bi Mugo.

Wapitanjia katika mtaa huo walifurahia kula mlo wa bure wakati huu ambapo bei ya vyakula ni ghali.

Mhudumu wa Tuktuk Bw Joseph Kinuthia, alisema chakula hicho ambacho ni cha bure, kitanufaisha familia yake.

Bw Kinuthia alifungiwa chapati sita za bure akabeba.

“Siku ya leo nimeshiba kwa kulishwa chapati na aina nyingine ya chakula bila malipo. Asubuhi nilipewa chapati sita ambazo nilipelekea familia yangu. Kila safari, ninapita na kuitisha moja. Saa hii wamenipa nyama,” alieleza Bw Kinuthia.

Pia, mama mboga katika mtaa huo alishindwa kuficha furaha yake kwenye uso wake baada ya kupewa chapati ale kabla ya kuendelea na kibarua chake.

“Chapati Festival wamefanya nikashiba leo. Sikuwa ninatarajia hao akina mama wa moyo wa kujali kwamba wangeniletea chakula hapa. Sijarudi kwa nyumba kupika,” akasema mwanamke huyo anayefanya kazi ya kufua nguo za wateja wake kujipa riziki.

Kundi hilo limekuwa likifanya hivyo kwa miaka kadhaa kuwatakia wakazi na wapitanjia sikukuu njema.

  • Tags

You can share this post!

Daktari aonya wanaume wa kuendea madoli

‘Kaeni chonjo watoto wasiingie kwa baa’

T L