• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Cleophas Malala aongoza UDA ‘kulinda’ mali ya wafanyabiashara Kakamega     

Cleophas Malala aongoza UDA ‘kulinda’ mali ya wafanyabiashara Kakamega    

NA SAMMY WAWERU

HUKU maeneo mbalimbali nchini Jumatano, Julai 19, 2023 yakishiriki maandamano ya upinzani, Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala aliongoza kundi la wafuasi wa chama hicho Kakamega kulinda biashara.

Akizungumza na wanahabari, Bw Malala alisema chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto kitajitolea kulinda mali ya wananchi.

“Ndio, tunatambua upinzani una haki Kikatiba kushiriki maandamano lakini si ya fujo. Sisi kama wana UDA tumejitolea kulinda mali ya Wakenya,” Katibu Mkuu huyo wa chama alisema.

Alikuwa ameandamana na kundi la vijana kutoka Kakamega.

Bw Malala aliwahi kuhudumu kama seneta wa kaunti hiyo.

“Hatutakubali uharibifu wa mali nchini,” Malala alionya.

Maandamano yanaendelea kushuhudiwa maeneo tofauti nchini, hasa ngome za muungano wa Azimio.

Kinara wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga aliitisha maandamano ya kitaifa katika kile alidai ni “kushinikiza serikali ya Kenya Kwanza kushusha gharama ya maisha inayozidi kulemea Wakenya”.

Upinzani pia umeweka masharti unaotaka yaafikiwe, ikiwemo kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kurejesha makamishna wa tume waliofutwa kazi na kujiuzulu kufuatia uchaguzi wa 2022, ikiwa ni pamoja na kutaka Mswada wa Kisheria wa Fedha 2023 kufutiliwa mbali.

Serikali ya Dkt Ruto hata hivyo imeharamisha maandamano hayo ya siku tatu kila wiki, kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

Bw Odinga, vinara na viongozi wenza Azimio, wamekaidi amri ya serikali.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya tulieni tuko na ‘plan’, asema Alfred...

Mzee adai polisi walimuumiza mgongo akitetea shamba lake

T L