• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Cristiano Ronaldo acheka na nyavu mara nne na kupitisha mabao 500 ligini

Cristiano Ronaldo acheka na nyavu mara nne na kupitisha mabao 500 ligini

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao manne katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na waajiri wake Al Nassr dhidi ya Al Wehda katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia (Saudi Pro League).

Magoli hayo yalimwezesha Ronaldo kufikisha zaidi ya mabao manne kitaaluma akitandaza soka katika ligi za klabu mbalimbali.

Ilimchukua Ronaldo dakika 40 pekee za mechi kati ya Al Nassr na Al Wehda kucheka na nyavu mara nne. Nyota huyo alihitimu umri wa miaka 38 mnamo Februari 5, 2023. Sasa amefunga mabao 503 ligini akivalia jezi za klabu tano za ligi tofauti.

Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa taji la Ballon d’Or alijiunga na Al Nassr mnamo Disemba 2022 kwa ujira wa Sh27 bilioni kwa mwaka.

Hata hivyo, hakuanza kampeni zake kambini mwa Al Nassr kwa matao ya juu jinsi ilivyotarajiwa. Alifunga bao moja pekee kupitia penalti kutokana na mechi tatu za kwanza akivalia jezi za kikosi hicho.

Ronaldo aliagana na Manchester United mnamo Novemba 2022 akijivunia kufungia miamba hao jumla ya mabao 103 katika kipindi cha awamu mbili.

Alipachika wavuni mabao 311 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) akichezea Real Madrid na akafunga magoli 81 zaidi akiwajibikia Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Aidha, alifungia Sporting Lisbon mabao matatu katika Ligi Kuu ya Ureno. Sporting ndicho kikosi kilichompokeza Ronaldo malezi ya soka.

Mabao manne yaliyofungwa na Ronaldo mnamo Alhamisi yalirejesha Al Nassr kileleni mwa jedwali la Saudi Pro League kwa wingi wa mabao. Wana alam sawa na nambari mbili Al Shabab ambao wametandaza mchuano mmoja zaidi wa akiba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hamza Anwar aanza Mbio za Magari Uswidi bila nuksi

‘Waititu hafai kusafisha mito jijini Nairobi’

T L