• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
CTWOO: Shirika lawafaa wengi kwa kusambaza chakula mitaa ya mabanda

CTWOO: Shirika lawafaa wengi kwa kusambaza chakula mitaa ya mabanda

Na SAMMY WAWERU

MOYO wa kutoa ulichangia pakubwa hatua ya Bi Dianah Kamande kuanzisha shirika moja lisilo la kiserikali (NGO) la kuwashughulikia wajane na mayatima la Come Together Widows and Orphans Organization (CTWOO).

CTWOO ni shirika linaloangazia na kusaidia vilevile waathiriwa wa dhuluma za kijinsia.

Janga la Covid-19 linaendelea kusambaratisha uchumi hapa nchini Kenya na ulimwengu kwa jumla, ambapo biashara nyingi zimeathirika kwa kiasi kikuu, idadi kubwa ya watu wakipoteza nafasi za kazi.

Waathiriwa wengi wanategemea vibarua vya kila siku na hali ya mkwamo wa baadhi ya shughuli hasa za juakali na biashara hizo imeathiri mapato na familia nyingi zinashinda na hata kulala njaa.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, CTWOO imejituma kutoa na kusambaza bidhaa za kula na mahitaji ya kimsingi katika mitaa ya mabanda.

Dianah ambaye pia ni mjane anasema linalenga kusaidia wajane, manusura wa vita vya kijinsia, mayatima, wagonjwa na wakongwe wasiojiweza kote nchini, wakati huu ambapo janga la corona linaendelea kuhangaisha na kutesa.

“Kwa sababu ya amri ya kuingia na kutotoka Nairobi, tuna timu ya wawakilishi wetu katika kila kaunti kusambaza misaada ya chakula na bidhaa za kimsingi,” Dianah anasema.

Kufikia sasa, CTWOO imeweza kufikia karibu familia 100 zinazoishi mitaa ya mabanda na Dianah anadokeza kwamba shirika hilo linalenga zaidi ya familia 500.

Dianah Kamande (kulia) akitangamana na wajane wenzake wakati wa kusambaza misaada ya chakula kufuatia athari za Covid–19. Picha/ Sammy Waweru

Aidha, linasambaza mchele, unga wa mahindi na wa ngano, majanichai, mafuta ya kupika, chumvi, bidhaa za kula zilizokaushwa na kuongezwa thamani ili kudumu muda mrefu, miongoni mwa bidhaa nyinginezo muhimu, pamoja na mahitaji ya kimsingi kama vile sodo.

Wakati wa mahojiano na Bi Dianah wakati akisambaza vyakula mitaa ya mabanda ya Babadogo na Chieko jijini Nairobi, aliambia Taifa Leo kwamba kufikia sasa CTWOO imetoa msaada wa bidhaa zenye thamani zaidi ya Sh100,000.

Mitaa mingine iliyofaidika kupitia ukarimu wa shirika hilo ni pamoja na Korogocho, Kiambiu na Ngomongo.

“Tunazingatia taratibu na maagizo ya Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya Covid-19. Aidha, tunashirikisha maafisa wa polisi katika shughuli hii nzima, na mitaa isiyoingilika kwa sababu ya utovu wa usalama tunatumia afisi za machifu na manaibu wao kutoa misaada. Huu ndio wakati ambao kama Wakenya wazalendo tunapaswa kujali wenzetu kwa kuwasaidia,” Dianah akasema.

Ili kufanikisha malengo ya CTWOO, Dianah alisema wanategemea mapato yao binafsi na ufadhili kupitia wasamaria wema.

“Katika kipindi hiki kigumu tumepata mfadhili wa hivi punde, Global Fund for Widows, shirika tunaloshirikiana kuhakikisha tunaafikia maazimio yetu, waathiriwa wapate chakula,” akaeleza, Millie Okombo mshirika akipongeza waliojitokeza kupiga jeki CTWOO.

Waliopokea misaada walikuwa na kila sababu ya kutabasamu, kufuatia ukarimu wa shirika hilo.

“Tunaombea CTWOO na waanzilishi wake heri njema, baraka na Mungu awajaalie mema. Kwa niaba ya wenzangu tunashukuru sana,” akasema mama mmoja mjane katika mtaa wa Chieko, Kasarani.

Licha ya jitihada za shirika hilo, halijakosa changamoto za hapa na pale.

“Katika visa kadhaa, wahudumu wetu wameporwa bidhaa na wahuni katika mitaa yenye utovu wa nidhamu na usalama, ndiposa tunashirikisha idara ya usalama kwa karibu,” Dianah anasema.

CTWOO ni shirika lililozinduliwa Septemba 2013.

“Wengi wanaopoteza wachumba, jamaa na marafiki huonekana wakati wa matanga na mazishi pekee, rambirambi zikiwa ‘salamu za pole, tutaonana hivi karibuni’, katu hakuna atakayeonekana tena. CTWOO ni kama boma linalopokea waathiriwa, pia mayatima na wahasiriwa wa dhuluma za kinyumbani ili kuwapa afueni maishani,” Dianah anafafanua.

Ni shirika linalotumika kama ukumbi na mtandao wa waathiriwa kujieleza, shabaha ikiwa kutetea haki zao na kuwahamasisha, ikiwa ni pamoja na kutoa mawaidha na wosia kuondoa jakamoyo.

Mbali na hayo, CTWOO pia huwasajili kupata kozi za mafunzo mbalimbali hasa za kiufundi, ili kuwaimarisha kibiashara na kimaisha.

Bi Millie Okombo (kulia), Mwenyekiti Tawi la Come Together Widows and Orphans Organization-Babadogo akiwa katika shughuli ya kusambaza misaada ya chakula kufuatia athari za Covid–19. Picha/ Sammy Waweru

Isitoshe, huwahimiza kubuni makundi ili kupata mikopo ya serikali, isiyotozwa riba.

“Makundi hayo huyaunganisha na maafisa wa Uwezo Fund, Women Enterprise Fund na Affirmative Action Fund (NGAAF), kupitia ushirikiano wetu, ambapo hupata mikopo isiyotozwa riba wawekeze katika biashara na kujiimarisha kimaendeleo,” Dianah anaelezea.

Aliasisi shirika hilo baada ya kushuhudia kisa cha mama mjane aliyechemsha mawe Mombasa, kwa sababu ya ukosefu wa chakula. CTWOO imeweza kuimarisha maisha ya zaidi ya familia 65, ambazo sasa zinaweza kujitegemea.

Ni kupitia jitihada zake, hata kabla kubuni CTWOO, mwaka 2012 Dianah alitambuliwa na Rais (mstaafu) Mwai Kibaki, ambapo alipokea tuzo ya kiongozi wa taifa, HSC, inayopokezwa walioafikia makuu katika jamii.

Mama huyo pia ametambuliwa katika ngazi ya kimataifa.

Huku akiendeleza juhudi za kutoa misaada wakati huu mgumu wa Covid-19, Dianah ana ujumbe kwa Wakenya;

“Kila mmoja awe ndugu mlinzi wa mwenzake. Wanaojiweza wajitokeze kusaidia wasiojiweza, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye hutujaalia na kutubariki kwa njia tofauti.”

You can share this post!

Kuchezea Gor Mahia lilikuwa ni kosa kubwa, asema mvamizi wa...

COVID-19: Visa 15 zaidi vyathibitishwa nchini idadi jumla...

adminleo