• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Digrii: Afueni kwa Jumwa korti ikikataa ombi la kumzuia kuwania

Digrii: Afueni kwa Jumwa korti ikikataa ombi la kumzuia kuwania

PHILIP MUYANGA NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ameshinda awamu ya kwanza ya kesi inayopinga azma yake ya kuwania ugavana wa Kilifi.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu ya Mombasa kukataa kutoa agizo la muda kuzuia Tume ya Uchaguzi (IEBC), kumjumuisha kwenye orodha rasmi ya mwisho ya wagombeaji kiti hicho.

Jaji Olga Sewe, wakati uo huo aliagiza pia kesi hiyo ihamishwe hadi Mahakama ya Malindi kwa kuwa kuna kesi nyingine kama hizo zinazohusu Mombasa, na zote zinahitajika zikamilishwe kwa wakati unaofaa.

Maafisa wa shirika lisilo la kiserikali la Concern Citizen Kenya, Bw Rajab Menza na Bw Daniel Chengo, wanataka Bi Jumwa azuiwe kuwania ugavana Kilifi wakidai hana cheti cha digrii.

Kupitia kwa wakili wao, Bw Derrick Odhiambo, walitaka mahakama itoe agizo la muda ili Bi Jumwa asiwe kwenye orodha itakayochapishwa katika gazeti rasmi la serikali kwani hilo litafifisha kesi yao.

Wakili Danstan Omari anayemwakilisha mbunge huyo, alipinga ombi hilo huku pia akisema walalamishi walifahamu vyema yeye ni mgombeaji kiti Kilifi ilhali walipeleka kesi Mombasa.

Kwa upande mwingine, IEBC kupitia kwa wakili Sheila Muthee, pia ilipinga ombi hilo kwa msingi kuwa ilishawasilisha pingamizi kuhusu kesi hiyo kusikilizwa mahakamani kwani, kulingana na tume hiyo, mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi aina hiyo.

Mbali na suala la digrii, walalamishi wamedai pia kuwa, Bi Jumwa aliyepewa tikiti ya chama cha UDA, hajahitimu kuwania ugavana wakidai kwamba amekiuka sheria za maadili ya uongozi wa umma.

Kwingineko, mgombeaji wa ugavana Kaunti ya Kilifi kupitia chama cha ODM, Bw Gideon Mung’aro, amemshutumu Naibu Rais William Ruto kwa kudai kuwa ni yeye aliyemwajiri katika serikali ya Jubilee baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Dkt Ruto akiwa katika kampeni zake wikendi alidai kuwa yeye ndiye aliyeshawishi kuajiriwa kwa Bw Mung’aro kama waziri msaidizi wa ardhi.

“Nilimpa hiyo kazi kwa miaka mitano na alishindwa kumaliza matatizo ya ardhi hapa. Mtu kama huyu akiomba kazi nyingine atapewa kweli?” Dkt Ruto alisema katika mkutano wa hadhara Kaloleni.

Hata hivyo, Bw Mung’aro alikana madai hayo akisema aliajiriwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Anawadanganya Wapwani akisaka kura. Anatumia jina langu baada ya kuona kuwa wakazi wa Kilifi hawamwamini tena,” akasisitiza.

  • Tags

You can share this post!

‘Cohen alilazimika kumuoa Sarah ili asirudishwe kwao’

Polisi waanza uchunguzi baada ya ofisi ya ‘Jicho Pevu’...

T L