• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
DNA yafichua wanaopigania mtoto si wazazi halisi

DNA yafichua wanaopigania mtoto si wazazi halisi

NA KATE WANDERI

Ilikuwa hali ya mshangao mkubwa kwa wanawake wawili kortini baada ya uchunguzi wa DNA kubaini kwamba, mtoto wa miezi miwili waliokuwa waking’ang’ania si wao.

Mtoto huyo alidaiwa kuibwa katika mtaa wa Kaptembwa, Nakuru.

Wawili hao, mmoja kutoka Busia na mwingine kutoka Nakuru wamekuwa wakikabiliana kwenye kesi mahakamani kuhusu malaika huyo lakini matokeo ya DNA yaliyowasilisha jana yalionyesha kwamba, hakuna yeyote kati yao ambaye alijifungua mtoto huyo.

Matokeo hayo sasa yanaibua maswali zaidi kuhusu mzazi halisi wa mtoto huyo mdogo huku Lilian Auma ambaye alishukiwa kumuiba akikabiliwa na madai ya ulanguzi wa watoto.

Uchunguzi huo wa DNA ulifanywa na mtaalamu Pamella Okello, Agosti 26 kwenye maabara ya serikali baada ya chembechembe za damu kuchukuliwa kutoka wanawake hao Lilian Auma, Ms Collend Mwajuma na mtoto huyo Sheila Sitindo.

“Bi Lilian Auma na Bi Collend Mwajuma si mama mzazi wa Sheila Sitindo,” ikaeleza sehemu ya ripoti ya DNA.

Bi Mwajuma alidai mwanawe alitoweka Julai 1 baada ya kumwacha akilala kwenye kochi nyumbani kwake Kaptembwo. Kulingana naye, mtoto huyo ni mwanawe wa pili na alikuwa amemwacha ili kuenda kununua chakula cha mchana cha kumpikia mumewe David Aura.

Bw Aura, ambaye ni seremala alieleza kushtuka kwake mkewe alipowasili baadaye na kumuuliza alikokuwa mwanao na hapo ndipo wakaanza kumtafuta kwa majirani na nyumba za karibu.

Mmoja wa majirani hata hivyo alimpasulia mbarika kwa kumwaambia alimwona mwanamke fulani akitoroka akiwa amembeba ‘mwanawe’ na mwishowe wakaelekea Busia baada ya jirani huyo kumwambia alikuwa na habari muhimu za kumsaidia kumpata.

Wakiwa wameandamana na polisi, walisafiri hadi Busia Julai 11 na kumpata Bi Lilian Auma nyumbani kwake kijiji cha Lukosi, Teso Kusini akiwa na mtoto ambaye Bi Mwajuma alidai ni wake.

Bila kuhojiwa, Bi Auma alinyakwa na kusafirishwa hadi Nakuru kisha akazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kaptembwo huku akikabiliwa na madai ya kumwiba mtoto wa wenyewe.

Alipohojiwa Bi Auma ambaye ni mkewe mwanajeshi wa KDF alisema alijifungua mtoto huyo kwa rafikiye mjini Nakuru kabla ya kurejea kwake Busia na akakanusha kumuiba kutoka kwa Bi Mwajuma.

Ingawa hivyo, imebainika kwamba amekuwa mke kwa miaka 16 lakini bado hajajaaliwa mtoto hali ambayo inazua maswali zaidi kwenye utata wa kupotea kwa mtoto wa Bi Mwajuma.

Korti sasa inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo Oktoba 14.

You can share this post!

Waliofurushwa Mau wapewe ardhi – Wabunge

Tajiri azushia pasta kunyimwa kiti kanisani

adminleo