• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Dunia yaomboleza Papa wa zamani wa Kanisa Katoliki Benedict XVI

Dunia yaomboleza Papa wa zamani wa Kanisa Katoliki Benedict XVI

NA MASHIRIKA

VATICAN CITY, VATICAN

HALI ya majonzi imetanda kote duniani leo Jumamosi kufuatia kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Benedict XVI.

Papa Benedict alifariki akiwa na umri wa miaka 95 katika makazi yake maalum mjini Vatican yaliko makao makuu ya kanisa hilo.

Aliliongoza kanisa hilo kutoka 2005 hadi 2013, alipojiuzulu kutokana na kudorora kwa hali yake ya afya.

Ndiye alikuwa Papa kwa kwanza kujiuzulu kwa karne kadhaa, baada ya Papa Gregory XII, aliyejiuzulu 1415.

Benedict aliishi maisha yake ya mwisho katika Nyumba ya Watawa ya Mater Ecclesiae, iliyo Vatican.

Mrithi wake, Papa Francis, alisema amekuwa akimtembelea mara kwa mara.

Yakasema makao ya Vatican kwenye taarifa: “Kwa masikitiko makubwa, ningependa kuwafahamisha kuwa Papa Mstahiki, Benedict XVI ametuacha leo saa 3.34 asubuhi katika Nyumba ya Watawa ya Mater Ecclesiae, Vatican.”

“Tutatoa maelezo zaidi,” yakaeleza makao hayo.

Vatican ilisema kuwa mwili wa Papa huyo utawekwa katika kanisa la St Peter’s Basilica kutoka Jumatatu “ili kusalimiwa na washirika wa kanisa hilo.”

Makao yalisema yatatoa mipango ya mazishi yake siku zitakavyoenda.

Kufuatia kifo chake, viongozi mbalimbali duniani wameanza kutuma risala za rambirambi.

Kiongozi wa kanisa hilo nchini Uingereza na Wales, Kadinali Vincent Nichols, amesema Papa Benedict alikuwa “mmoja wa viongozi wa kidini wenye ushawishi zaidi katika karne ya 20”.

Akasema kwenye taarifa: “Ninakumbuka wakati Papa alizuru eneo hili 2010. Tuliona unyenyekevu wake na makaribisho yake kwa kila mmoja. Alikuwa mtu mwadilifu, msomi na mtumishi aliyemkaribia Mungu daima.”

Ijapokuwa Papa huyo wa zamani amekuwa akiugua kwa muda, Kadinali Nichols amesema hali yake ya afya ilidorora kutokana na umri wake mkubwa.

Mnamo Jumatano, Papa Francis aliwarai washirika wa kanisa hilo katika Vatican “kusali maombi maalum kwa ajili ya Papa Benedict”, aliyesema alikuwa mgonjwa sana.

Papa huyo alizaliwa nchini Ujerumani mnamo Aprili 16, 1927 kama Joseph Ratzinger.

Mnamo 2005, aliibukia kuwa miongoni mwa mapapa wazee zaidi kuwahi kuchaguliwa kuliongoza kanisa hilo, kwani alikuwa na umri wa miaka 78.

Wakati alipohudumu kanisa hilo lilikuwa likikabiliwa na madai ya mapadre kuwalawiti watoto.

Mapema mwaka 2022, kiongozi huyo alikubali makosa hayo yalifanyika na akaomba msamaha kuhusu vile masuala hayo yalishughulikiwa wakati alihudumu kama askofu wa Munich kati ya 1977 na 1982.

  • Tags

You can share this post!

Msichana aliyepotea apatikana amefariki nyumbani kwa...

WALIOBOBEA: Sally Kosgei: Alikuwa balozi mzalendo mwenye...

T L