• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Eddie Nketiah atia saini mkataba mpya wa miaka mitano kambini mwa Arsenal

Eddie Nketiah atia saini mkataba mpya wa miaka mitano kambini mwa Arsenal

Na MASHIRIKA

EDDIE Nketiah, 23, atakuwa miongoni mwa washambuliaji tegemeo kambini mwa Arsenal msimu ujao baada ya kutia saini mkataba mpya wa miaka mitano utakaomshuhudia akitia mfukoni ujira wa Sh15 milioni kwa wiki.

Fowadi huyo aliyekuwa katika mwaka wa mwisho wa kandarasi yake ugani Emirates, amewajibishwa na Arsenal mara 92 na akapachika wavuni mabao 23 tangu alipoanza kuvalia jezi za kikosi cha kwanza mnamo 2017.

Nketiah anayetarajiwa kujaza pengo la Alexandre Lacazette aliyerejea Olympique Lyon ya Ufaransa muhula huu, alikamilisha kampeni za msimu wa 2021-22 kwa matao ya juu huku akifungia waajiri wake mabao matano katika mechi nane za mwisho.

“Nimefurahishwa na hatua ya Nketiah kuhiari kusalia nasi. Amejitolea kuitumikia Arsenal kadri ya uwezo wake. Amedhihirisha ukubwa wa uwezo wake uwanjani na sasa tutamtegemea pakubwa katika safu ya mbele muhula ujao,” akasema kocha Mikel Arteta kwa kusisitiza kuwa Arsenal wanaendelea kujisuka upya.

Kadri wanavyolenga kurejea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2017, Arsenal wana mpango wa kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji kwa kujinasia maarifa ya Gabriel Jesus kutoka Manchester City na Leicester City.

Kikosi hicho tayari kimeafikiana na FC Porto kuhusu uhamisho wa kiungo Fabio Vieira, 22, hadi ugani Emirates kwa Sh5 bilioni. Vieira, alitawazwa Mchezaji Bora wa kipute cha Euro U-21 mwaka uliopita.

Alifunga mabao sita na kuchangia mengine 14 kutokana na mechi 27 za Ligi Kuu ya Ureno mnamo 2021-22 na akasaidia Porto kutwaa ubingwa wa kivumbi hicho. Atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Arsenal msimu huu baada ya kipa raia wa Amerika, Matt Turner na fowadi chipukizi kutoka Brazil, Marcus Vinicius Oliveira Alencar almaarufu Marquinhos.

Nketiah aliyekuwa na jezi nambari 30 ugani Emirates, sasa atavalia jezi nambari 14 iliyowahi kuwa ya washambuliaji matata wa Arsenal – Thierry Henry (1999-2007, 2012) na Piere-Emerick Aubameyang (2018-2022).

Alifunga magoli mawili dhidi ya Norwich City kwenye Carabao Cup katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Arsenal mnamo 2017 na akawa sehemu ya kikosi kilichoshinda Kombe la FA na taji la Community Shield mnamo 2020.

Kufikia sasa, Nketiah ndiye mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Uingereza cha U-21. Ana mabao 16 kutokana na mechi 17 na alikuwa nahodha wa kikosi kilichosaidia Uingereza kutwaa taji la Euro kwa chipukizi wa U-21 mwaka jana.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

UJAUZITO NA UZAZI: Athari za mimba kuharibika

PENZI LA KIJANJA: Ni sharti upige muhuri ndoa yako!

T L