• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Eintracht Frankfurt wafalme Uropa

Eintracht Frankfurt wafalme Uropa

NA MASHIRIKA

SEVILLE, Uhispania

ILIKUWA raha kwa Eintracht Frankfurt na karaha kwa Glasgow Rangers baada ya Ligi ya Uropa kukamilika kwa ushindi wa klabu hiyo ya Ujerumani kwa njia ya penalti 5-4 ugani Ramon Sanchez-Pizjuan, Jumatano.

Frankfurt, ambayo ni klabu ya kwanza ya Ujerumani kutawala dimba hilo, haikupoteza mchuano katika kampeni yake.

Ilisakata mechi 13 ikizoa ushindi saba ikiwemo kuzima miamba Barcelona na West Ham, pamoja na kutoka sare mara sita.

Frankfurt, ambayo imeshinda mashindano ya Bara Ulaya tangu Uefa Cup mwaka 1980, pia ilijikatia tiketi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao kwa mara ya kwanza tangu 1960.

Katika ushindi wa Jumatano, Frankfurt ilikuwa bora kwa kipindi kikubwa, hasa katika dakika 45 za kwanza.

Hata hivyo, ilitangulia kufungwa bao katika dakika ya 57 kupitia kwa Joe Aribo. Hiyo ni baada ya makipa wote wawili Allan McGregor (Rangers) na Kevin Trapp (Frankfurt) kupangua makombora kadhaa hatari.

Aribo alipata goli walinzi wa Frankfurt walipochanganyikiwa.

Mabeki wa Rangers pia walichangia katika bao la kusawazisha waliposita kuondosha krosi ya Filip Kostic iliyosukumwa wavuni na Rafael Borre dakika ya 69. Rangers iliponea krosi nyingine hatari kutoka kwa Kostic dakika ya 89.

Katika dakika 30 za nyongeza, pande zote zilipata nafasi kadhaa nzuri, ingawa Trapp aliwazima Ryan Kent na James Tavernier.

Trapp, ambaye aliibuka mchezaji bora wa fainali, alipangua penalti ya Aaron Ramsey wakati wa mikwaju ya kuamua mshindi.

Frankfurt ilifunga penalti zake zote. Kilikuwa kilio kambini mwa Rangers.

Kocha Giovanni van Bronckhorst alisema, “Nimesikitika sana. Tulikaribia sana… Nilikuwa na wakati mbaya kama huo nilipokuwa mchezaji ikiwemo kupoteza fainali ya Kombe la Dunia. Inauma sana.”

  • Tags

You can share this post!

Boga sasa abadili mgombea mwenza

Jopo kuamua hatima ya jaji Chitembwe

T L