• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Elijah Manangoi apigwa marufuku ya miaka miwili kwa hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli

Elijah Manangoi apigwa marufuku ya miaka miwili kwa hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za mita 1,500 Elijah Manangoi amepigwa marufuku ya miaka miwili kwa hatua ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Mnamo Julai 23, 2020, Kitengo cha Maadili (AIU) katika Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kilimzuia Manangoi kushiriki mashindano yoyote baada ya kupatikana na hatia ya kutojiwasilisha vinara wa AIU ili afanyiwe vipimo vya kubaini iwapo alishiriki matumizi ya pufya.

Hata hivyo, AIU kwa sasa imempata Manangoi na hatia ya kutumia pufya na imempokeza marufuku ya miaka miwili kuanzia Disemba 22, 2019 hadi Disemba 21, 2021. Disemba 22, 2019 ndiyo tarehe ambapo Manangoi alikataa kujiwasilishwa kwa vipimo kwa mara ya tatu mfululizo.

“Matokeo yote yaliyosajiliwa na Manangoi kwenye mashindano aliyoshiriki baada ya Disemba 22, 2019 yamefutiliwa mbali. Aidha, anapokonywa mataji, tuzo na medali zote alizopokezwa kuanzia kipindi hicho,” ikasema sehemu ya taarifa ya AIU.

Manangoi alikuwa amekosa kufanyiwa vipimo vya kubaini matumizi ya pufya kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia Julai 3, 2019, Novemba 12 na Disemba 22.

Katika kujitetea kwake, Manangoi alisema kwamba mnamo Julai 2, 2019 alikuwa jijini Frankfurt akishughulika kuhusu jinsi ya kusafiri hadi Nairobi. Baada ya kukosa ndege ya kwanza, Manangoi alisema alilazimika kusubiri na hivyo akawasili Nairobi saa tano usiku mnamo Julai 2019.

Aidha, alisema kwamba mzigo aliokuwa nao ulisahaulika San Francisco na hivyo, asingeweza kufika nyumbani kwake kwa kuwa ufunguo wa nyumba ulikuwa kwenye mzigo huo uliomfikia baada ya makataa ya kufanyiwa vipimo katika eneo la Rongai.

Hata hivyo, maelezo ya Manangoi hayakuridhisha vinara wa AIU ambao walitilia shaka sababu za mtimkaji huyo kukosa hata kujiwasilisha kwao siku iliyofuata ya Julai 3, 2019 wala kuwafafanulia kuhusu masaibu yaliyomkuba safarini.

Kuhusu sababu ya kukosa vipimo vya Novemba 12, Manangoi alisema kwamba alirejea nyumbani usiku sana kwa sababu yeye ni afisa wa polisi na alihitajika kushika doria usiku. Baada ya doria, alichelewa barabarani kutokana na msongomano wa magari na hivyo akashindwa kusafiri hadi eneo alikotarajiwa kufanyiwa vipimo.

Katika tukio la tatu, mtimkaji huyo alisema kwamba alikuwa na jeraha alilokuwa akiliuguza kuanzia Agosti 27, 2019 na mnamo Disemba 2019, alikuwa amesafiri hadi Austria kufanyiwa tathmini zaidi ya jeraha hilo.

Manangoi anakuwa mwanariadha wa pili wa haiba kubwa nchini Kenya kupigwa marufuku chini ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya bingwa wa London Marathon mnamo 2017, Daniel Wanjiru, kupigwa marufuku ya miaka minne kwa kukiuka kanuni za pufya.

AIU ilikuwa awali imemsimamisha Wanjiru kushiriki mashindano yoyote kuanzia Aprili 14, 2020 baada ya chembeche za dawa haramu kupatikana kwenye sampuliza damu yake. Alipigwa marufuku mnamo Oktoba 15.

Jopo la Nidhamu la AIU lilitangaza mnamo Januari 6, 2021 kwamba adhabu ya Wanjiru, 28, ilianza kutekelezwa Disemba 9, 2019 na hivyo matokeo yote ya mashindano aliyoyashiriki kuanzia Machi 2019 yakafutiliwa mbali.

Wanariadha tisa wa Kenya wameadhibiwa na AIU kwa makosa mbalimbali katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Kati ya hao, wawili ni washindi wa zamani wa London Marathon.

Mbali na Wanjiru, Wilson Kipsang aliyeshinda London Marathon mnamo 2012 na 2014 pia alipigwa marufuku ya miaka minne baada ya kukosa kujiwasilisha kwa minajili ya vipimo vya AIU.

Adhabu ya Wanjiru ilitolewa wiki tatu baada ya mwanariadha mwingine wa masafa marefu Patrick Siele aliyeambulia nafasi ya 12 kwenye mbio za Venloop Half Marathon nchini Uholanzi kupigwa marufuku ya miaka mitatu na wiki sita. Siele pia aliibuka bingwa wa Cardiff Half Marathon nchini Uingereza mnamo 2019.

Awali, Philip Kangogo ambaye ni mwanariadha wa masafa marefu alikuwa amepigwa marufuku ya muda ya miaka miwili..

Siele na Kangogo wanajiunga na orodha ndefu ya wanariadha wa Kenya ambao wamepigwa marufuku kwa kipindi cha kati ya miaka miwili na minane kwa hatia ya kukiuka kanuni za pufya.

Mercy Kibarus alipigwa marufuku ya miaka minane mnamo Septemba 2019 kwa hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli huku Kenneth Kipkemoi na Alex Oloitiptip wakipigwa marufuku ya miaka miwili kila mmoja kwa matumizi ya pufya na kutojiwasilisha kwa vipimo vya afya mtawalia.

Wengine ambao wamepigwa marufuku ya miaka minne kila mmoja ni Mikel Kiprotich Mutai, Vincent Kipsegechi Yator na Peter Kwemoi baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Kati ya wanariadha ambao bado wanasubiri hatima yao mwezi huu baada ya kudaiwa kukiuka kanuni za pufya ni James Kibet na Alfred Kipketer aliyeibuka bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2014.

  • Tags

You can share this post!

Mwanariadha Alfred Kipketer apigwa marufuku kwa kukiuka...

Gor Mahia wapewa Napsa Stars ya Zambia kwenye mchujo wa...