• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ELIMU MSINGI: Binti mfumaji mazulia

ELIMU MSINGI: Binti mfumaji mazulia

CHARLES WASONGA na PIUS MAUNDU

BINTI Abigael Mumo, ambaye ni mwanafunzi wa gredi ya tatu katika Shule ya Msingi la Kaluluini, Kaunti ya Machakos, amevutia watu wengi kutokana na talanta yake ya kipekee ya ushonaji wa mazulia madogo ya milangoni (door mats).

Mbali na kushona, msichana huyu amekirimiwa kipaji cha kurembesha mazulia hayo kwa maandishi na michoro mbalimbali ya maua maridadi. Ubora wa mazulia anayoyatengeneza unakaribia viwango vya mazulia yanayoundwa kitaalamu viwandani.

“Ushonaji wa mazulia ni sanaa ya kupendeza. Hata hivyo, kazi hii inahitaji uangalifu na umakinifu mkubwa mno,” anasema.

Abigael hukata vipande vya magunia ya nailoni yenye ukubwa unaohitajika. Kisha kwa kutumia sindano aina ya krocheti na nyuzi nono pamoja na pamba, yeye hushona mazulia ya kila aina kwa urahisi akiwa nyumbani kwao Kaluluini viungani mwa mji wa Matuu.

Hufanya hivyo kila mara baada ya kukamilisha vipindi vya masomo shuleni. Msanii huyu ambaye ni kitinda mimba katika familia ya watoto sababu, anasema alijifunza ushonaji wa mazulia kwa kusoma kitabu kiitwacho ‘Mwanasayansi’ kwa zaidi ya miezi kumi shule zilipofungwa mwaka jana baada ya mlipuko wa korona.

Alivutiwa na kitabu hicho siku moja alipoandamana na babake, Bw John Kyalo, katika duka moja la vitabu mjini Matuu na akamsihi amnunulie.

“Nilianza kushona hatua kwa hatua, nikifuata mwongozo kitabuni na nikafaulu,” anaeleza kwa tabasamu.

“Abigael huhitaji siku tano kukamilisha zulia moja ikiwa hana kazi nyingi za shuleni. Kupitia usanii wake, sasa nyumba yetu imepambwa sana tofauti na nyinginezo kijijini, ” anaungama mamake, Bi Rose Karimi.

You can share this post!

TAHARIRI: Hotuba ya Uhuru ichochee kuondoa ubaguzi na...

PAUKWA: Biashara Haramu ya Titi (sehemu 5)

T L