• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
FA: Mashabiki wa Manchester United kuganda na Arsenal

FA: Mashabiki wa Manchester United kuganda na Arsenal

NA MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa klabu ya Manchester United katika maeneo mengi ya Mlima Kenya, wameapa kuunga mkono timu ya Arsenal ikiingia ugani mnamo Jumapili, Januari 7, 2024, dhidi ya Liverpool katika kipute cha Kombe la FA.

Arsenal itachapana na Liverpool katika kipute cha kombe la FA raundi ya tatu kuanzia saa moja na nusu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani katika uga wa Emirates.

Hii ni licha ya mashabiki wa Arsenal nao kuwa na wasiwasi kwamba huenda wakumbane na kichapo kibaya sana kimo cha maangamizi iwapo hao wa Man U watawaunga mkono.

“Ikiwa kuna uungwaji mkono hatuhitaji kwa sasa ni wa mashabiki wa Man U. Huenda wakaleta nuksi tupu na tukapokezwa kichapo. Hata afadhali Chelsea watuunge mkono… Man U wakae tu na huruma wao hatuutaki,” akasema Lydiah Mburu, ambaye ni shabiki sugu wa Arsenal mjini Murang’a.

Hata hivyo, wafuasi wa Man U wameambia Taifa Leo kwamba licha ya uhasama wanaokuwa nao dhidi ya Arsenal, klabu ya Liverpool nayo huwa na dharau.

“Mimi siwezi kamwe nikasahau jinsi ambavyo Liverpool mnamo Machi 5, 2023, ilituaibisha kwa kutupokeza kichapo cha magoli 7 kwa nunge,” akasema Stephen ‘Chicharito’ Muraya akiwa mjini Karatina.

Katika mechi hiyo Gakpo alifunga mawili katika dakika za 43 na 50, Núñez akamuiga kwa kujipa mawili katika dakika za 47 na 75, Mo’ Salah akajipa yake mawili katika dakika za 66 na 83 huku Firmino akiwaondoa ugani kwa goli la dakika ya 88.

Stephen Kamau kutoka mji wa Thika akiongea katika kituo cha redio cha Coro FM alisema: “Mimi huwa naomba Mungu itokee timu ambayo itapiga Liverpool mabao hata 10 kwa nunge ili tujioshe aibu hiyo ya 7-0.”

Alisema kwamba Man U ilionjesha Arsenal magoli 8-2 mnamo Agosti 28, 2011, “kwa hivyo hao wanatujua sisi ni hatari lakini wakiweza kutupigia Liverpool binafsi nitaokoka hata nifunge kilemba ikibidi”.

Naye Martin Kung’u akipiga simu kutoka mtaa wa Kahumbu ulioko eneobunge la Kigumo, alisema kwamba ataunga mkono Arsenal “kwa kuwa Liverpool ilitukabidhi aibu ya zaidi ya miaka 90 ilipoturambisha magoli hayo saba bila jibu”.

Man U ilikuwa imepoteza kwa kiwango sawa na hicho dhidi ya Wolverhampton mwaka wa 1931, nao mwaka wa 1895 ikipoteza dhidi ya Liverpool kwa mabao 7-1.

Arsenal walitoka sare ya 1-1 mnamo Desemba 23, 2023, walipokutana katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na watakutana tena Februari 4, 2024, katika mchuano wa raundi ya pili wa ligi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Demu ajiondoa kwa chamaa cha vidosho wanyemeleaji wa mabwana

Wakenya wanaoishi Venezuela wataka kifo cha padri raia...

T L