• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Gakuyo ahimiza wafuasi wake wafuate ngoma ya Azimio la Umoja

Gakuyo ahimiza wafuasi wake wafuate ngoma ya Azimio la Umoja

Na LAWRENCE ONGARO

ASKOFU David Kariuki Gakuyo wa kanisa la Calvary Chosen Centre Church lililoko mjini Thika amejitosa ulingoni kupigia debe vuguvugu la Azimio la Umoja.

Bw Gakuyo aliyetangaza kwamba anawania kiti cha ubunge cha Thika, amewarai wafuasi wake wafuate ngoma ya Azimio la Umoja.

Mnamo Jumatano, Askofu huyo aliendesha mkutano mkubwa katika uwanja wa Thika Stadium, huku watu kutoka makabila na tabaka zote wakifurika uwanjani kusikiliza ajenda zake na mipango aliyo nayo kwa wakazi wa Thika.

Haya yanajiri huku kukiwa na msisimko kwa sababu kinara wa ODM Raila Odinga, anatarajiwa kuzuru mjini Thika mnamo Jumamosi.

Askofu Gakuyo amewarai wakazi wa Thika wajitokeze kwa wingi ili kumkaribisha Raila.

Ameeleza kwamba mipango ya Azimio ni pamoja na kuboresha maisha ya kila Mkenya kwa kuwaunganisha pamoja.

Alieleza kuwa ana uhakika kuwa Raila ana nia njema na wananchi wa Kenya hasa wa Mlima Kenya kutokana na jinsi anavyonyenyekea kwao.

Alisema anataka kupewa kura kwa sababu yeye ni mzaliwa wa kijiji cha Munyu, umbali wa kilomita saba kutoka mji huo.

“Lengo langu kuu litakuwa kuona ya kwamba pesa za maendeleo za NG-CDF zinatolewa bila ubaguzi wowote,” alifafanua Askofu Gakuyo.

Alieleza wakati wa kura kila mmoja ana uhuru wa kumchagua kiongozi ampendaye bila kujazwa uwoga eti “ufuate mwelekeo fulani.”

Alisema ajenda nyingine muhimu ambayo atajihusisha nayo ni kuhakikisha wakazi wanapata maji safi hasa wale wa maeneo ya Makongeni, Kiganjo, na Landless mjini Thika.

You can share this post!

AFCON: Mali yapiga Tunisia katika mchuano wa Kundi F...

Gambia waanza kampeni za AFCON kwa matao ya juu baada ya...

T L