• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:50 AM
Hali ngumu kuandama Wakenya 2022

Hali ngumu kuandama Wakenya 2022

Na BENSON MATHEKA

JAPO 2022 ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini, Wakenya watakuwa wakifuatilia kwa karibu masuala yanayoathiri maisha yao moja kwa moja kama Mlima wa Madeni ya serikali yanayofanya maisha yao kuwa magumu na mkondo ambao janga la corona litachukua.

Haya ni miongoni mwa masuala ambayo Wakenya wanasema yataathiri maisha yao mwaka huu wa mpito Rais Uhuru Kenyatta atakapoondoka mamlakani Agosti 2022 baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

Huku janga la corona likiendelea kuathiri sekta zote za maisha na aina mpya ya Omicron ikitatiza juhudi zilizopigwa kuangamiza virusi hivyo, wizara ya afya itakuwa na kibarua cha kuhakikisha imechanja Wakenya 27 milioni mwaka huu 2022 ilivyoahidi.

Katika sekta ya afya, Wakenya pia watakuwa wakifuatilia kuona iwapo serikali itatimiza ahadi yake ya afya kwa wote moja ya Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenya ambayo iliyumba mwaka 2021.

Ajenda nyingine ni ujenzi wa nyumba za bei nafuu, utengenezaji wa bidhaa na utoshelevu wa chakula.

Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wa afya kwa wote unaendelea huku ikipanga kufanyia mabadiliko Bima ya Taifa ya Afya na kusajili Wakenya 19.5 milioni katika UHC kufikia mwisho wa mwaka huu 2022.

Tayari Wakenya 5.1 milioni maskini na walio kwenye hatari wametambuliwa kwa mpango huo.

Katika mwaka huu wa 2022, Wakenya wanafuatilia kwa makini kuona iwapo watapata afueni baada ya kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi mwaka 2021 hali ya uchumi ilipodorora kutokana na sera za serikali na janga la corona.

Wengi hawana ajira baada ya corona kusambaratisha sekta kadhaa za uchumi ikiwemo ya utalii inayoajiri maelfu ya Wakenya.

Dalili zimeonyesha kuwa utakuwa mwaka mgumu baada ya kampuni za bima kupandisha bima za magari kwa asilimia 50.

Wataalamu wa uchumi wanasema hatua hii, pamoja na kupanda kwa bei za mafuta, kutaongeza gharama ya uchukuzi na kufanya maisha kuwa magumu kwa Wakenya.

“Kumbuka kwamba kuna mlima wa madeni ya zaidi ya Sh8 trilioni yanayopaswa kulipwa,” asema mtaalamu wa masuala ya uchumi, Bw Peter Kimotho.

Tayari serikali inaendelea kukopa mabilioni kutoka Shirika la IMF kufadhili bajeti yake katika mpango unaoendelea kwa miezi 38 kuanzia Aprili 2021 hadi 2024.

Mbali na mikopo ya IMF, serikali inaandaa mkopo mpya wa Eurobond unaotarajiwa katika miezi sita ijayo kufadhili mapengo katika bajeti.Kenya pia inalipa mikopo ya awali ya Eurobond na kutoka serikali ya China iliyotumia kwa miradi ya miundomsingi.

Utakuwa mwaka ambao wazazi wanatarajiwa kubeba mzigo zaidi huku mtaala wa elimu wa CBC ambao wanatarajiwa kujukumika zaidi ukiingia awamu muhimu ya Gredi ya Sita na sekondari.

Mwaka huu, sekta ya elimu itafuatiliwa zaidi huku kukiwa na mitihani miwili ya KCPE na KCSE ndani ya mwaka mmoja.

  • Tags

You can share this post!

UDAKU: Essien na mkewe Akosua Puni wamerejesha tena mahaba

Watakaopigwa darubini kali 2022

T L