• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Harry Kane aanza kampeni ya Bundesliga kwa matao ya juu

Harry Kane aanza kampeni ya Bundesliga kwa matao ya juu

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Uingereza, Harry Kane, alifunga bao na kuchangia jingine katika mchuano wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ulioshuhudia waajiri wake Bayern Munich wakipepeta Werder Bremen 4-0 ugenini, Ijumaa.

Kane alimwacha hoi kipa Jiri Pavlenka katika dakika ya 74 na kupachika wavuni bao la pili la Bayern waliopata magoli mengine kupitia kwa Mathys Tel na Leroy Sane aliyecheka na nyavu mara mbili.

“Nilikuwa na wasiwasi kidogo hasa ikizingatiwa kwamba ilikuwa mechi yangu ya kwanza katika Bundesliga. Tulianza vizuri kwa kufunga bao la haraka mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na hilo likanipa msukumo zaidi,” akasema Kane.

Akihojiwa na wanahabari, Kane alikiri kuwa ushindi huo dhidi ya Bremen ulimpa faraja zaidi baada ya Bayern kuanza muhula vibaya kwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa RB Leipzig kwenye gozi la German Super Cup mnamo Agosti 12, 2023.

Kane anatarajiwa kujaza kikamilifu pengo la kigogo wa Poland, Robert Lewandowski, aliyeagana na Bayern zaidi ya mwaka mmoja uliopita na kutua kambini mwa Barcelona.

Ingawa Bayern walinyanyua taji la Bundesliga mnamo 2022-23 baada ya kupiku Borussia Dortmund kwa pointi moja, alama 71 walizojizolea ndizo chache zaidi kwao kuwahi kujikusanyia ligini tangu 2010-11 walipoambulia nafasi ya tatu jedwalini.

Kane anatazamiwa kuchezea Bayern kwa kipindi cha miaka minne ijayo baada ya kukatiza uhusiano wake wa muda mrefu na Spurs kwa kima cha Sh15.6 bilioni.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alibanduka Spurs akiwa mfungaji bora wa kikosi hicho baada ya kupachika wavuni mabao 280 kutokana na mechi 435.

Aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara tatu – 2015-16, 2016-17 na 2020-21. Akijivunia mabao 213 kutokana na mechi 320 katika EPL, alihitaji magoli 48 zaidi kuvunja rekodi ya nguli Alan Shearer ambaye ni mfungaji bora wa muda wote katika historia ya kipute hicho.

Ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Uingereza kwa mabao 58 na aliibuka pia mfungaji bora katika fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi baada ya kucheka na nyavu mara sita. Hata hivyo, hajawahi kunyanyua taji lolote la haiba kubwa katika ngazi ya klabu au timu ya taifa.

Bayern walijizolea taji lao la 33 la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu jana. Ilikuwa mara yao ya 11 mfululizo kutwaa kombe hilo na wamenyanyua pia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara sita na German Cup mara 20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

AMINI UKIPENDA: Kijiji Marsabit ambako wakazi waliamka na...

Ajivunia kuwa askari wa kaunti baada ya kiwango cha elimu...

T L