• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Historia bei ya petroli ikigonga Sh134

Historia bei ya petroli ikigonga Sh134

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA watakabiliwa na wakati mgumu baada ya serikali kuongeza bei ya mafuta kuwa kiwango kikubwa kulingana na bei mpya iliyotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta Kawi Nchini (EPRA).

Katika bei ilitangazwa Jumanne, Septemba 14, 2021 bei ya mafuta aina ya petrol sasa itauzwa kwa Sh134.72 kwa lita jijini Nairobi na viungani baada ya bei yake kuongezwa kwa Sh7.58. Bei ya bidhaa hii imesalia Sh127.14 kwa lita kwa miezi miwili iliyopita ya Julai na Agosti ambapo serikali ilichelea kuongeza bei.

Kulingana na mwongozo wa bei hiyo mpya iliyotangazwa na Eptra bei ya dizeli imepanda kwa kima cha Sh7.94 huku mafuta ikipanda kwa Sh12.97, mtawala kuanza Jumatano. Hii ina maana kuwa dizeli itauzwa kwa Sh107.66 jijini huku mafuta taa inayotegemewa na Wakenya wengine wenye mapato ya chini itauzwa kwa Sh110.82 kwa lita moja jijini Nairobi.

Bei hizi mpya zitakuwa juu katika miji iliyoko mbali na Nairobi kwa sababu bei za bidhaa hizi ukadiriwa kulingana na umbali kutoka Mombasa ambako shehena ya bidhaa hizo hutua katika Bandari ya Mombasa.

Petroli, dizeli na mafuta zimekuwa zikiuzwa kwa Sh127.14, Sh107.66 na Sh97.85 kwa miezi miwili iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Kiptoo Bargoria alisema asasi hiyo iliongeza bei ya mafuta mwezi huu baada ya serikali kuondoa nafuu (subsidy) ambayo serikali imekuwa ikitoa na ambayo imeokoa wateja.

“Nafuu katika bei ya rejareja kwa mafuta haijajumuishwa katika ukadiriaji wa bei ya mwezi huu ambayo itatumika kwa siku 30 hadi Oktoba 14, 2021. Hii ndio sababu iliyochangia bei ya bidhaa za mafuta kupanda,” Bw Kiptoo akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Hii ina maana kuwa Epra iliondoa nafuu ya Sh7.10 kwa bei ya mafuta, Sh9.9 kwa bei ya dizeli na Sh11.36 kwa bei ya mafuta taa, kwa kila lita.

“Bei iliyotangazwa mwezi huu pia inajumuisha ushuru ziada ya thamani (VAT) ya kima cha asilimia 8 kulingana na Sheria ya Fedha ya 2018, Sheria ya Ushuru iliyofanyiwa marekebisho 2020, na ushuru kwa bidhaa (Excie Duty) iliyofanyiwa marekebisho ili kuafiki viwango vya mfumko wa bei,kulingana na Ilani ya Kisheria Nambari 194 ya 2020,” akaongeza Bw Kiptoo kwenye taarifa.

Lakini Wakenya wamekuwa wakilalamikia mwendo wa serikali kutoza aina nyingi za ushuru kwa bidhaa za mafuta, hali inayochangia bei kupanda ikilinganishwa na mataifa jirani kama vile Uganda na Tanzania.

You can share this post!

Natembeya kuwania ugavana Trans Nzoia

CBC: Magoha apuuza malalamishi ya wazazi