• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Hofu ajira kupotea SGR ikifika Uganda

Hofu ajira kupotea SGR ikifika Uganda

NA ANTHONY KITIMO

MPANGO mpya wa serikali kuanzisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Naivasha hadi Kampala, Uganda, umewatia hofu wamiliki na wahudumu wa malori ya kusafirisha mizigo kutoka humu nchini.

Wafanyabiashara hao ambao hupeleka mizigo nchi za nje kutoka bandarini, wameeleza hofu kwamba reli ya SGR ikifikishwa Uganda, biashara zao zitafilisika na kusababisha ukosefu wa ajira kwa wengi.

Hayo yanajiri huku Uganda ikijitahidi kusafirisha asilimia 100 ya shehena kwa kutumia SGR kutoka Mombasa hadi Naivasha na kisha kutumia reli ya zamani hadi Malaba.

Hiyo ni sehemu ya makubaliano ya taifa hilo jirani na Kenya kupata fedha za kujenga reli ya kisasa ambayo inatarajiwa kuathiri vibaya mamia ya watu wanaotegemea usafiri wa barabarani.

Chama cha Wachukuzi wa Kenya (KTA) kilisema hawatakubali kurudi katika hali ambazo zilisababisha sheria kuwekwa kwa wenye biashara kubeba mizigo kwa lazima kwa njia ya reli.

“Sielewi ni kwa nini serikali inakopa pesa kusaidia usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani na wakati huo huo kulipia mkopo badala ya kuwezesha usafirishaji wa mizigo kwa haraka na madereva wanaolipa ushuru na kodi mbalimbali kwa nchi,” mwenyekiti wa KTA, Bw Newton Wang’ oo akasema.

Aliongeza, “Gharama ya biashara imezidi kwa kiwango cha juu, kwa hivyo serikali haipaswi kuzidisha hatua ambazo zitafanya bidhaa katika nchi jirani kuwa nafuu zaidi kuliko hapa.”

Wiki iliyopita, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda, Bw Edward Katumba Wamala, alisema serikali hizo mbili zilitia saini mkataba ambao pia utaongeza matumizi ya reli kusafirisha mizigo ya Uganda kwa reli kwa asilimia 100 miezi ijayo.

“Tumekuwa tukifanya vyema katika suala la kutumia reli za Kenya kusafirisha mizigo yetu na tunajitahidi kusaidia miundomsingi iliyopo kikamilifu huku tukiendelea kupanga kujenga ya kisasa,” akasema Bw Wamala.

Ahadi ya Uganda ya kutumia reli pia ni habari njema kwa serikali ya Kenya inayolenga kuongeza mapato ya kulipa mkopo wake na benki ya Exim ya China kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli ya SGR.Kufikia sasa, SGR kutoka Mombasa hadi Naivasha imefadhiliwa na China kwa gharama ya jumla ya Sh656.1 bilioni.

Ingawa serikali ya Kenya Kwanza iliondoa sheria iliyolazimisha usafirishaji wa mizigo kwa SGR wakati ilipoingia mamlakani, imebainika wafanyabiashara wengi bado wanapendelea reli kuliko malori.

Ripoti iliyotolewa hivi majuzi na Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS) ilionyesha kuwa, idadi ya wafanyabiashara wanaopendelea SGR kuliko malori kusafirisha shehena zao za mizigo inazidi kuongezeka.

Hii ni kutokana na kuwa, uchukuzi wa treni huchukua muda mfupi na ni salama kwa kiasi kikubwa ukilinganishwa na uchukuzi wa barabarani.

  • Tags

You can share this post!

NEMA yataka maoni yatolewe kuhusu ujenzi wa hoteli ya Raila

Vitisho vyachacha kati ya Azimio na Kenya Kwanza

T L