• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Hoki: Butali 3-bora Klabu Bingwa Afrika

Hoki: Butali 3-bora Klabu Bingwa Afrika

NA JOHN KIMWERE

WAFALME wa hoki nchini Butali Warriors walipiga Police Machine ya Nigeria mabao 3-2 na kumaliza namba tatu katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (ACCC) yaliyomalizika ugani Nairobi Union, Nairobi, jana Jumapili.

Katika kitengo cha wanawake, Vipusa wa GRA walitawazwa mabingwa kwa kuzoa alama 13, sawa na Army Ladies ya Ghana ila waliwapiku kwa tofauti ya idadi ya mabao.

Delta Queens ya Nigeria ilishika nambari tatu na alama 11, ikifuatiwa na Lakers ya Kenya.

Lakers ilifikia alama hizo baada ya kutoka sare tasa na Delta Queens ya Nigeria, japo ilihiari namba nne kwa tofauti chache ya mabao.

Blazers ya Kenya ilimaliza ya tano ilipoadhibiwa mabao 3-2 na Army Ladies.

Butali na Police zilivaana katika mchuano huo wa kuamua namba tatu baada ya kila mmoja kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mechi za Kundi A na B, mtawalia.

Butali ya kocha Zack Aura ilionyesha mechi safi ingawa wapinzani hao pia hawakulaza damu.

Raiz Rana alifungia Butali bao la kwanza dakika ya nane, Sunday Orinya akasawazishia Police dakika ya 37.

Dakika tisa baadaye Henry Jayeoba wa Police alifunga bao la pili nao Calvin Kanu na Festus Onyango wakaipa Butali bao kila mmoja dakika ya 53 na 55, mtawalia.

“Tulipania kubeba kombe mwaka huu lakini hatuna lingine ila kukubali yaishe,” alisema meneja wa Butali, Kamal Sembi.

Hata hivyo, alipongeza vijana wake kwa kupambana kiume na kumaliza katika nafasi ya tatu maana mechi hazikuwa mteremko.

“Sina shaka tulicheza kadri ya uwezo wetu ingawa hatukufanikiwa kutimiza azma yetu,” alisema nahodha wa Butali, Constant Wakhura.

Nao malkia wa mchezo huo nchini, Scorpions ya Strathmore University ilipigwa mabao 3-0 na Ghana Revenue Authority (GRA) ya Ghana na kumaliza katika nafasi ya sita kwa alama nne.

Tukienda mitamboni, fainali ya wanaume ilikuwa ikiendelea kati ya Sharkia ya Misrina Exchequers ya Ghana. Sharkia walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-2.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mwandishi anayelenga uanahabari

Liverpool yafufuka

T L