• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Idadi ya watu walioangamia kwenye mkasa wa moto Hawaii yagonga 106

Idadi ya watu walioangamia kwenye mkasa wa moto Hawaii yagonga 106

NA AFP

KAHULUI, Amerika

IDADI ya watu waliokufa katika mkasa mkubwa wa moto ulioanzia kwenye maeneo ya misitu katika mji mmoja wa jimbo la Hawaii, Amerika imegonga 106, maafisa wa utawala wamesema huku mochari za muda zikipanuliwa kukidhi idadi kubwa ya maiti.

Awali, Gavana wa jimbo hilo Josh Green alikuwa ameonya kuwa idadi ya wafu kutokana na moto huo, uliotokea kuanzia wiki jana, mjini Lahaina ingeongezeka.

Mkasa huo umetajwa kama mbaya zaidi wa moto kuteketeza misitu kutokea nchini Amerika.

Bw Green alisema maafisa wa Kaunti ya Maui wamekuwa wakitumia mbwa wa kunusa kusaka miili katika eneo la mkasa. Makontena yenye barafu yalikuwa yakitumika kama mochari za muda kuhifadhia maiti katika Kituo cha Polisi cha Kuchunguza Matukio katika Kaunti ya Maui Jumanne jioni, kulingana ripoti za wanahabari wa AFP.

Wakazi wa eneo hilo, ambalo ni kisiwa, waliohojiwa na AFP walionekana kujawa na hofu kuu kutokana na moto huo ulioanza wiki jana. Gavana Green alionya kuhusu jaribio lolote la watu fulani kunyakua ardhi katika maeneo yaliyotekea viungano wa mji wa Lahaina.

Hii ni baada ya wakazi kuelezea hofu kuhusu matajiri fulani kuwashawishi wawauzie vipande vya vya ardhi ili wajenge nyumba kubwa za kukodisha.

“Lengo letu ni kulinda jamii ya hapa huku tukiendelea na mipango ya kujenga upya makazi yaliyoharibiwa na moto,” akasema.

“Kwa hivyo, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa ardhi ya wakazi hazitwaliwi na watu kutoka nje,” Gavana Green akaongeza.

Shughuli za kutambua miili zinaendelea leo Jumatano, huku maafisa wakifichua kuwa walikuwa wamekosanya sampuli za chembechembe za DNA kutoka kwa watu 41 ambao jamaa zao haijulikani ni wapi waliko. Ni miili mitano pekee ambayo ilikuwa imetambuliwa kufikia leo Jumatano asubuhi huku maafisa kutoka Kaunti ya Maui wakitoa majina mawili baada ya kuwajulisha watu wa familia zao.

“Tunatoa rambirambi zetu kwa familia ambazo zimeanza kupokea ripoti kuhusu vifo vya wapendwa wao,” Meya wa Kaunti ya Mui Richard Bissen akasema kwenye taarifa.

Mkuu wa polisi wa kisiwa hicho alisema nyingi za miili hiyo imeteketea vibaya kiasi cha kutotambuliwa. Hii ni kwa sababu moto huo ulikuwa mkali zaidi.

Watu wanaendelea kuelezea jinsi walivyokwepa kifo kwa tundu la sindano huku baadhi yao wakiwalaumu watawala kwa kufeli kuwajulisha mapema kuhusu kuenea haraka kwa ndimi za moto huo.

Annelise Cochran ameambia AFP kwamba aliingiwa na matumaini pale maafisa waliposema moto mdogo uliotokea milimani ulikuwa umedhibitiwa Jumanne asubuhi.

Lakini moto huo ulienea ghafla na kuteketeza sehemu kubwa.

“Tuliona moshi ukifuko na anga ikageuka mweusi huku upepo ukivuma kwa kasi ya kilomita 140 kwa saa. Lilikuwa tukio la haraka na la kutamausha,” akasema Cochra, 30.

“Tuliona ndimi za moto na kujua kwamba zilikuwa zikitukaribia,” mwanamke huyo akasema, akiongea kuwa amri haikutolewa kwamba wahamie maeneo salama.

Baada ya kutoroka kwa gari alikumbana na msongamano wa magari yaliyoachwa na wenyewe walioamua kutoroka kwa miguu. Hapo ndipo Cochra akaamua kujitosa ndani ya bahari ili kujinusuru.

“Tulijizamisha ndani ya maji ili kujisalimisha. Tulikuwa tukipumua hewa ya bahari kwa sababu hewa ilikuwa imechafuliwa zaidi na moto huo,” mama huyo akaeleza.

Aliondolewa majini baada ya saa kadha.

  • Tags

You can share this post!

Uhispania kusubiri mshindi wa mechi kati ya Uingereza na...

Rais Ruto amtaka Mandago, wenzake wabebe msalaba kuhusu...

T L