• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Inter Milan guu moja ndani ya nusu-fainali za UEFA baada ya kupepeta Benfica 2-0

Inter Milan guu moja ndani ya nusu-fainali za UEFA baada ya kupepeta Benfica 2-0

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku alifunga penalti mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake Inter Milan kupepeta Benfica 2-0 katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku jijini Lisbon, Ureno.

Nicolo Barella aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao katika dakika ya 51 na kuwaweka miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa nusu-fainali ya UEFA msimu huu.

Benfica waliopania kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani walianza mechi kwa matao ya juu huku Rafa Silva akimwajibisha vilivyo kipa Andre Onana na beki matata raia wa Uholanzi, Denzel Dumfries.

Bao la Lukaku anayechezea Inter kwa mkopo kutoka Chelsea, lilitokana na penalti iliyosababishwa na Joao Mario aliyenawa mpira ndani ya kijisanduku.

Refa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Michael Oliver, aliwapa Inter penalti hiyo baada ya kuthibitisha tukio la Mario kunawa mpira kupitia teknolojia ya VAR.

Chini ya kocha Simone Inzaghi, Inter sasa wako pua na mdomo kutinga nusu-fainali za UEFA msimu huu kadri wanavyopanga kurudiana na Benfica ugani San Siro, Italia, mnamo Aprili 19, 2023.

Inter waliendea Benfica kwa mkondo wa kwanza wakiwa na kibarua kigumu cha kujinyanyua baada ya kutoshinda mechi yoyote kati ya sita za awali.

Benfica walidengua Club Brugge katika hatua ya 16-bora kwa jumla ya mabao 7-1 huku Inter wakitinga robo-fainali ya UEFA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12 kwa kung’oa FC Porto.

Benfica wamekuwa na fomu nzuri katika UEFA muhula huu, na walikamilisha kampeni za Kundi H kileleni baada ya kupiku Maccabi Haifa, Juventus na PSG walioaga kipute hicho katika hatua ya 16-bora mikononi mwa Bayern.

Mechi dhidi ya Inter ilikuwa yao ya 13 katika soka ya bara Ulaya msimu huu tangu waanze kutandaza kipute cha UEFA katika raundi ya tatu ya kufuzu mnamo Agosti 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanawake Shakahola walalamika kukosa kupachikwa mimba

Linturi apigwa breki na Zambia kwa uagizaji mahindi  

T L