• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Itikadi na miko ya Uswahilini ambayo haihusiani na dini

Itikadi na miko ya Uswahilini ambayo haihusiani na dini

Na HAWA ALI

WIKI jana tulizungumzia baadhi ya Imani na itikadi za Waswahili zenye mfungamano mkuu na dini ya Kiislamu. Hata hivyo, pamoja na imani hizo zinazoongozwa na misingi ya dini ya Kiislamu, Waswahili wana imani nyingine ambazo hazihusiani na dini ya Kiislamu.

Mathalan, mtu anapokula chakula au kunywa kitu halafu akapaliwa au kujiuma ulimi watu husema mtu huyo anatajwa/anasemwa vibaya na watu wengine.

Aidha, mtu anapotembea kisha akajikwaa mguu wa kulia, watu huamini anakoenda kuna heri, na ikiwa atajikwaa mguu wa kushoto basi anakoenda hakuna heri.

Mara nyingi ikiwa atajikwaa mguu wa kushoto hushauriwa avunje safari yake, ama aiahirishe aende baadaye.

Bundi na paka mweusi

Bundi anaaminika ni ndege mwenye nuksi. Ikiwa bundi atalia karibu na nyumba ya mtu au katika paa la nyumba basi mtu huyo hupatwa na msiba.

Huaminiwa kwamba bundi na paka mweusi huashiria mkosi. Kwamba ikiwa mtu atakutana na paka mweusi asubuhi, basi siku hiyo itakuwa yenye mkosi; huenda jambo baya litamtokea mhusika.

Mjamzito kutokula mayai

Itikadi nyingine ni kwamba mama mjamzito hapaswi kula mayai. Inaaminika kuwa ikiwa mwanamke mjamzito atakula mayai, basi atapata mtoto asiye na nywele.

Mojawapo ya makatazo kwa mwanamke mjamzito wa Kiswahili ni kuepuka kula mayai kadiri ya uwezo wake. Pia kumpitia mwanamke mjamzito na moto ni mwiko mkubwa kwani inaaminiwa ni kumkata uzazi.

Mama akikuvulia nguo

Ikiwa mama yako atakukasirikia na kukuonyesha sehemu zake za siri huku akisema maneno ya kukulaani basi huaminiwa kwamba utapatwa na laana na huenda ukawa na maisha mabaya au hata kurukwa na akili (kuwa mwendawazimu).

Imani kama hii ni maarufu si tu miongoni mwa jamii za Waswahili, bali pia katika jamii nyinginezo za Afrika.

Kula gizani

Mtu anayekula gizani hula na shetani. Hii pia ni imani maarufu katika jamii nyingi za Afrika.Kama tulivyotangulia kusema, hakika imani kama hizi hazihusiani na dini. Na labda hatuwezi kuthibitisha uhusiano wa ishara na athari au matokeo ya imani hizi kisayansi.

Lakini bila shaka, imani hizo ni sehemu ya utamaduni wa watu, na kila jamii huwa na imani zake.Huenda imani hizo zinalenga kuzuia wanajamii kutofanya mambo fulani ambayo wanayaona si maadilifu au ni jitihada ya kujaribu kueleza mambo au matokeo au hali wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Wawaniaji urais walipe uzito suala la...

‘Jicho Pevu’ ashambulia familia ya Gavana Joho