• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 12:47 PM
Jamal Musiala ateua kuchezea Ujerumani badala ya Uingereza au Nigeria

Jamal Musiala ateua kuchezea Ujerumani badala ya Uingereza au Nigeria

Na MASHIRIKA

FOWADI chipukizi wa Bayern Munich, Jamal Musiala, ameteua kuchezea timu ya taifa ya Ujerumani badala ya Uingereza na Nigeria alizokuwa pia na uwezo wa kuziwajibikia kwenye soka ya kimataifa.

Sogora huyo anayetimu umri wa miaka 18 mnamo hapo kesho Ijumaa ya Februari 26, 2021, alifunga bao lake la kwanza kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kusaidia Bayern kupepeta Lazio ya Italia 4-1 kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa kipute hicho mnamo Februari 23, 2021.

Musiala ambaye alizaliwa mjini Stuttgart, Ujerumani, amewahi pia kuwakilisha Uinegreza na Ujerumani katika soka ya kiwango cha chipukizi. Kwa mujibu wa sogora huyo, tayari amewazia “sana” kuhusu mustakali wake wa usogora kwenye ulingo wa kimataifa.

“Ni wapi pazuri zaidi kwa ajili ya mustakabali wangu kitaaluma? Ni wapi nilipo na nafasi nzuri za kucheza sana?” akajibu Musiala wakati wa mahojiano kati yake na gazeti la Athletic nchini Ujerumani.

“Mwishowe, ilinilazimu Kusikiliza hisia zangu ambazo kwa muda mrefu ziliniamisha kwamba maamuzi bora zaidi ni kusalia Ujerumani, nilikozaliwa. Kwa kweli, yalikuwa maamuzi mazito na magumu,” akasema mshambuliaji huyo.

“Nina mapenzi makubwa kwa Ujerumani, na ninavutiwa sana na Uingereza. Ni mioyo miwili ambayo yote imekuwa ikipiga ndani yangu,” akaongeza Musiala.

Musiala ambaye alihamia Uingereza baada ya kupokezwa malezi ya soka nchini Ujerumani akiwa mtoto, aliwahi pia kuchezea akademia ya Chelsea kabla ya kujiunga na Bayern mnamo 2019.

Amewakilisha Uingereza katika soka ya Uingereza katika timu ya taifa ya chipukizi wa U-21. Alifunga bao katika ushindi wa 5-0 uliosajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Albania mnamo Novemba 2020.

Musiala kwa sasa anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Jaochim Loew wa timu ya taifa ya Ujerumani kwenye mechi za Machi 2021 kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kisa cha mwigizaji Omosh kifungue wasanii macho na...

MBIO ZA NYIKA: Mabingwa kusubiri zaidi kutetea taji