• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Jimi Wanjigi amtaka Rais Kenyatta ajitetee kuhusu ‘kashfa’ ya Sh25.2 trilioni

Jimi Wanjigi amtaka Rais Kenyatta ajitetee kuhusu ‘kashfa’ ya Sh25.2 trilioni

NA MWANGI MUIRURI

[email protected]

MWANIAJI wa urais kwa tiketi ya chama cha Safina Bw Jimi Wanjigi, Jumamosi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta atoe taarifa ya kibinafsi kuhusu jinsi ambavyo serikali yake imetekeleza bajeti za Sh17 trilioni ambazo ameandaa kupitia Wizara ya Fedha katika kipindi cha miaka tisa iliyopita.

Vile vile, alimtaka Rais Kenyatta atoe taarifa nyingine kwa Wakenya kuhusu Sh8 trilioni ambazo Wakenya wanabeba kwa sasa kama mkopo wa kitaifa na pia kuhusu Sh200 bilioni ambazo zilikopwa nchini Amerika mwaka wa 2014.

Bw Wanjigi alidai kuwa mkopo huo kutoka Amerika ulitoweka na kuishia kwa mifuko ya watu binafsi. Kwa ujumla, taarifa ambayo Bw Wanjigi alidai inajumlisha Sh25.2 trilioni.

Bw Wanjigi akiwa mjini Murang’a alisema kuwa rais ndiye kinara wa serikali na anafaa aelezee ni kwa nini uchumi wa kitaifa ni matambara licha ya Wakenya kulipa ushuru kwa dhati na kwa kujituma ili wapate utawala utakaoinua hali ya maisha.

Alisema kuwa serikali ya Jubilee kwa sasa imefilisika na rais anafaa kutoa taarifa kuhusu ni kwa nini pato la kitaifa halijakuwa likipanda,

Wakenya wakizama kwa shida za ukosefu wa ajira na umaskini unaofanya watembee wakiwa na haya na hata wengi kupata msongo wa mawazo.

Alimkumbusha rais Kenyatta kuwa alipochukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais mstaafu Mwai Kibaki, Wakenya 38 kati ya 100 ndio walikuwa na njaa lakini idadi hiyo kufikia sasa imepanda hadi 68 kati ya 100.

“Rais anafaa kutupa jibu. Tunataka tupewe taarifa kuhusu gharama ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ili Wakenya waelewe ni kwa nini mradi huo hauna faida hadi sasa licha ya kuwaweka katika lindi la madeni ya Kichina,” akasema.

Alisema kuwa mwaka wa 2014 serikali ilikopa Sh300 bilioni.

“Sh200 bilioni zilikopwa kutoka kwa benki ya Kimarekani kwa jina Chase Morgan Stanley na Sh100 kutoka kwa benki ya Citi. Hizo za Citibank ziliwekwa katika hazina ya kitaifa lakini zile Sh200 bilioni hazijawahi kuonekana katika taarifa zozote za serikali licha ya kuwa sisi Wakenya ndio tunalipa kama mkopo ulio na riba. Rais anafaa kutupa taarifa kuhusu hilo,” akasema.

Bw Wanjigi alisema kuwa wakati Afisi ya Mhasibu Mkuu wa serikali ilijaribu kuuliza swali kuhusu mkopo huo wa Sh200 bilioni, na akataka kusafiri hadi nchini Amerika kufuatilia pesa hizo, serikali kupitia mitandao yake ya utawala ilizima kwa vitisho jitihada hizo.

“Rais anafaa kutuelezea kwa utaratibu na kwa takwimu za kueleweka jinsi zilivyotumika pesa hizo za mikopo ambayo kwa sasa imetinga Sh8 trilioni na kukiwa na mpango wa kuzidisha hadi trilioni 12. Wakenya wanaumia wakilipa madeni kwa sasa lakini manufaa ya kukopa hayaonekani,” akasema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Jeremiah Kioni alimtaja Bw Wanjigi kama mfanyabiashara ambaye anakabiliwa na kesi tele kortini na nyingi ni kuhusu ulaghai.

“Ningetaka Wakenya wafahamu kuwa anayedai kuwa kuna kashfa serikalini kuhusu uadilifu wa matumizi ya fedha yeye mwenyewe yuko mahakamani akijitetea kuhusu ulaghai. Huu ni msimu wa siasa na tutasikia mengi kutoka kwa wapinzani,” akasema.

Alisema kuwa miradi ya mabilioni ya pesa haswa katika ujenzi wa barabara, ujenzi wa mitambo ya reli, ujenzi wa bandari na pia usambazaji maji na umeme ilifanyika kwa kiwango kikuu katika utawala wa Rais Kenyatta.

Bw Kioni aliongeza kuwa kwa sasa walio katika mrengo wa hasla wanataka taarifa kutoka kwa rais Kenyatta kuhusu kila aina ya madai “lakini wao wote walichaguliwa sambamba na rais Kenyatta ndani ya chama tawala cha Jubilee na wanaompigia debe awe rais wa tano wa taifa hili akiwa ni Dkt William Ruto ndiye naibu wa rais katika serikali hiyo.”

Alisema kuwa Dkt Ruto alichaguliwa sambamba na rais Kenyatta “na kwa kuwa ndiye Bw Wanjigi na washirika wake wanafuata kama kinara wao ndani ya serikali ya Jubilee, huyo ndiye mfaafu zaidi wa kuwajibu kuhusu tetesi zao za utendakazi wa serikali.”

Alimtaka Bw Wanjigi kwanza ajitakase kuhusu madai tele dhidi yake kabla ya kuanza ‘kumpaka tope’ Rais Kenyatta.

 

  • Tags

You can share this post!

Kenya Open ya kulenga shabaha kwa bastola yavutia nchi 10

Ugavana: Askofu Margaret Wanjiru sasa akubali Sakaja...

T L