• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
JSC kuamua majaji 11 wanaofaa kwa Mahakama ya Rufaa

JSC kuamua majaji 11 wanaofaa kwa Mahakama ya Rufaa

Na SAM KIPLAGAT

TUME ya Huduma za Mahakama imekamilisha shughuli ya kuhoji majaji wanaotaka kujaza nafasi 11 katika Mahakama ya Rufaa.

Majaji waliofika katika mahojiano hayo walitakiwa kutoa msimamo wao kuhusu masuala tata kama vile uavyaji mimba, haki za mashoga, umri unaofaa kwa vijana kuanza kujihusisha na masuala ya mapenzi na uhalalishaji wa bangi.

Majaji hao walikuwa na kibarua kigumu kufafanua hukumu walizotoa hapo awali.

Tume hiyo ya watu 11 pia ilitaka majaji waliohojiwa kuelezea maoni yao kuhusu ugavi wa mali wanandoa wanapotalikiana na mbinu mbadala za kutatua mizozo nje ya mahakama.

Watu 35 walihojiwa katika mahojiano hayo yaliyodumu kwa wiki mbili na sasa tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu David Maraga itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa majaji 11 watakaoteuliwa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuna usawa wa kijinsia.

Jaji Maureen Onyango, msimamizi wa mahakama ya kutatua mizozo ya waajiri na wafanyakazi alisema kuwa amekuwa akitofautiana na Mahakama ya Rufaa inapotoa uamuzi wa kupunguza fidia iliyotolewa na mahakama ya chini bila kutoa sababu.

“Kuna wakati mwingine ambapo ninahisi kutofautiana na Mahakama ya Rufaa haswa inapoamua kupunguza fedha za fidia iliyoagizwa na mahakama ya chini ilipwe bila kutoa sababu ya kufanya hivyo,” akasema.

Jaji Onyango alisema Mahakama ya Rufaa inafaa kuwa na jaji aliye na ufahamu kuhusu mizozo ya wafanyakazi ili kuhakikisha kuwa inatoa maamuzi yanayofaa.

Jaji Pauline Nyamweya, msimamizi wa Mahakama ya Masuala ya Kikatiba, Milimani jijini Nairobi, alikataa pendekezo la kutaka bangi ihalalishwe huku akisema madhara ya bangi ni mengi kuliko faida.

“Hata bangi ikihalalishwa kwa ajili ya matibabu hospitalini?” akauliza Jaji David Majanja mmoja wa wanajopo.

“Bado imepigwa marufuku. Mimi nikiwa jaji naangalia madhara ya muda mrefu ya bangi,” akasema Jaji Nyamweya.

Jaji Jessie Lesiit wa Kitengo cha Jinai katika Mahakama Kuu, alisema ngono miongoni mwa vijana wa umri mdogo inafaa kuhalalishwa kwa sababu watoto wanaojihusisha na mapenzi mapema wana tabia mbaya na wala halifai kuwa kosa.

Jaji Lessit alisema watoto wanaoshtakiwa kwa kushiriki mapenzi na wenzao wanafaa kupewa ushauri nasaha badala ya kukamatwa.

Dkt Imana Laibuta, wakili na mhadhiri aliambia JSC kuwa Wakenya hawafai kukimbia kukumbatia utamaduni wa watu wengine kwa sababu ni maarufu katika nchi nyingine alipoulizwa kuhusu msimamo wake kuhusiana na haki za mashoga.

Hata hivyo, Dkt Laibuta alisema ikiwa sheria itabadilishwa na ushoga kuhalalishwa atahakikisha sheria inatekelezwa kikamilifu.

Wakili Paul Lilan aliambia Tume kwamba madai kuwa Idara ya Mahakama ndiyo inatatiza vita dhidi ya ufisadi hayana mashiko.

Profesa Nixon Sifuna Wanyama, mtaalamu wa sheria ya mazingira, alijimiminia sifa huku akisema kuwa yeye ni msuluhishaji wa utata.

Dkt Kipkoech Chebii, mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo cha Moi alisema kuwa atakuwa kiungo muhimu katika Mahakama ya Rufaa haswa katika kesi zinazohusiana na mazingira.

You can share this post!

ODM yafifia Jubilee ikivuna ngome zake

Wito Nakuru ipandishiwe hadhi kuwa jiji

adminleo