• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Raila ndiye baba wa ugatuzi, apewe urais 2022 – Junet

Raila ndiye baba wa ugatuzi, apewe urais 2022 – Junet

Na SAMMY WAWERU

BW Raila Odinga ndiye “baba” wa ugatuzi Kenya na serikali ikiwa mikononi mwake itakuwa salama.

Hii ni kulingana na mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed ambaye ameendelea kupigia upatu kiongozi huyo wa ODM akisema anaelewa kwa kina changamoto zinazowakumba Wakenya.

“Raila Odinga ndiye baba wa ugatuzi, Katiba na uhuru wa kuwepo kwa vyama vingi nchini. Anafaa kuongoza Kenya kutokana na mchango wake mkubwa kuiboresha,” Bw Junet akasema akizungumza jijini Nairobi.

Chini ya utawala wa serikali ya mesto, iliyoongozwa na Rais mstaafu, Mwai Kibaki, Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu alikuwa miongoni mwa waliounga mkono Katiba ya sasa kupitishwa.

Ilizinduliwa mwaka wa 2010, na kuanza kutumika 2013. Ni kufuatia Katiba hiyo, serikali za ugatuzi na zinazoongozwa na magavana zilizinduliwa. Junet anaendeleza kampeni za Waziri huyo Mkuu wa zamani kuingia Ikulu mwaka ujao, licha ya matamshi yake ya hivi punde na ambayo yamezua tumbojoto kwa wapinzani wa Bw Raila.

Akiongea katika hafla ya mchango eneo la Nyamira, iliyoongozwa na Bw Raila na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Junet alikejeli endapo Raila atatwaa serikali 2022 “itakuwa ya Nyanza”.

Mchango huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, Junet kwenye tani zake akidai jamii ya anakotoka Kagwe imeridhia uongozi kwa zaidi ya miaka 20. Alisema Kagwe atakuwa akizuru Nyanza kama mgeni. Ni matamshi ambayo yamepokelewa kwa uzito na hamaki, hasa kwa wapinzani wa Bw Odinga.

UDA, chama kinachohusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, wandani wake kutoka Mlima Kenya wamemkashifu vikali Junet kufuatia mtelezo wake wa ulimi. Akijitetea, mbunge huyo hata hivyo amesisitiza kwamba matamshi yake yalitafsiriwa vibaya.

“Baba (akimaanisha Raila Odinga) akiniona ama aniskie nikieneza jumbe za chuki na uchochezi atanipiga marufuku chamani. Baba ndiye bora kuongoza taifa hili,” Junet akasema.

Bw Raila na Naibu wa Rais, Dkt Ruto ni kati ya viongozi na wanasiasa ambao wametangaza nia yao kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao. Wawili hao wamekuwa wakiandaa mikutano ya umma sehemu mbalimbali nchini, katika mchakato mzima kurai Wakenya kuwapigia kura.

Aidha, kila mgombea anatoa ahadi na kuuza sera zake kuboresha uchumi, kuondoa umaskini, kuimarisha sekta mbalimbali na kutafutia vijana ajira. Kwa upande wake Raila, ameahidi kuendeleza na kupiga jeki ugatuzi akihoji zinalenga kufikishia wakazi wa mashinani huduma za serikali.

You can share this post!

Inasikitisha ni wahudumu 10 pekee wa afya wamefuzu...

Sudi alitumia vyeti feki kuingia serikalini, mahakama...

T L