• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kagame akataa zigo la wakimbizi wa DRC

Kagame akataa zigo la wakimbizi wa DRC

NA AL JAZEERA

KIGALI, RWANDA

RAIS wa Rwanda Paul Kagame amesema serikali yake haitatoa tena hifadhi kwa wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ukosefu wa utulivu na usalama mashariki mwa DRC Congo imewalazimisha wengi kuvuka mpaka na kuingia Rwanda.Rais huyo alisema kwamba serikali yake haitabeba mzigo wa kuhifadhi wakimbizi hao.

“Watu kukimbia makazi yao na kuvuka mpaka na kuingia Rwanda sio tatizo letu. Serikali yangu haitabeba mizigo kama hiyo,” akasema Bw Kagame.

Kulingana na rais huyo, tishio la usalama ni kile alichoelezea kama mabaki ya vikosi vya Wahutu wenye itikadi kali ambao walijaribu kuliangamiza kabila lake la Kitutsi katika mauaji ya kimbari ya 1994.

Rwanda inashutumiwa kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 jambo ambalo nchi hiyo imekuwa ikikanusha.

Kundi hilo la waasi limeteka maeneo mengi katika miezi ya hivi karibuni, jambo lililowafanya wengi kukimbilia maeneo salama kwa kuvuka mpaka na kuingia Rwanda.

Novemba 2022, Umoja wa Mataifa ulisema takriban wakimbizi 72,000 wa Congo wamevuka na kuingia nchini Rwanda.

Nchi ya Kigali inalaumu Kinshasa kwa mgogoro huo na kuishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kufumbia macho madai ya DRC ya kuunga mkono chama cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), vuguvugu la waasi wengi wa Wahutu wa Rwanda waliohusishwa na mauaji ya kimbari mwaka wa 1994 nchini Rwanda.Kigali inachukulia FDLR kama tishio linalohalalisha uvamizi wa DRC.

Rwanda pia imeishutumu DRC kwa kutumia mzozo huo kwa malengo ya kisiasa na vile vile ‘kutekeleza’ mauaji ya Novemba ya angalau raia 131.

Novemba 2022, Rais mtaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta na Kagame walikubaliana kuhusu haja waasi wa M23 kukomesha vita na kuondoka maeneo waliyoteka mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kulingana na taarifa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenyatta na Kagame walikubaliana, kwa njia ya simu, kwamba hatua hiyo ndio itatoa nafasi kwa kupatikana amani ya kudumu DRC.

“Wawili hao walikubaliana kwamba ili amani ipatikane DRC sharti pande zote mbili zisitishe vita kwanza. Awamu ya pili ya mazungumzo ya amani itafanyika jijini Luanda, Angola wiki ijayo,” EAC ikasema kwenye taarifa.

“Watu watakuwa wakisubiri ikiwa kweli M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC wanasimamisha vita,” mwandishi wa habari wa shirika la Al-Jazeera, Malcom Webbe, alisema akiripoti kutoka mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi la M23 lilitia saini mkataba wa amani na serikali ya DRC mnamo 2013 kwa ahadi kwamba wapiganaji wake wangeshirikishwa katika jeshi la kitaifa nchini humo.

Hata hivyo, kundi hilo lilianza vita tena mwishoni mwa 2021 kwa sababu ya kile walidai ni hatua ya serikali ya DRC kudinda kutimiza ahadi ya 2013.

Wapiganaji wa kundi hilo wametekeleza mashambulio matatu makubwa mashariki mwa DRC tangu Machi 2022.

Katika shambulio walilotekeleza mwanzoni mwa Oktoba 2022, mamia ya watu walikufa na wengine zaidi ya 200,000 kutoroka makazi yao.

  • Tags

You can share this post!

Patrick ‘Jungle’ Wainaina asema ni vyema Kawira...

CECIL ODONGO: Gachagua si Naibu Rais wa eneo la Mlima Kenya...

T L