• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kandanda: Gundi ya mshikamano, silaha dhidi ya mihadarati

Kandanda: Gundi ya mshikamano, silaha dhidi ya mihadarati

NA LABAAN SHABAAN

KITUO cha kukuza vijana wenye kipaji cha soka cha Talanta Africa Football Academy (Tafa), kimevutia watoto wa kati ya umri wa miaka mitano hadi matineja wa umri wa miaka 19 katika kijiji cha Kasarani, eneobunge la Gilgil, Kaunti ya Nakuru.

Mwasisi wa Tafa na Mkurugenzi wa Michezo Bw Sammy Kamau, anaeleza kuwa lengo la kuasisi kituo hicho mwaka 2019 lilikuwa kudhibiti mambo mambo mabaya na kuzima uhuni na matumizi ya dawa za kulevya katika jamii.

Bw Sammy Kamau akiwa katika maktaba ya Talent Africa Football Academy Kasarani, Gilgil. PICHA | LABAAN SHABAAN

Anadokeza mambo haya yanayoibuka kwenye misingi ya kukosa elimu yanajumuisha matumizi ya mihadarati na mimba na ndoa za utotoni.

Tafa inasaidia jamii kukabili shida zao kupitia kukuza talanta ya kandanda, stadi za kompyuta, hamasa ya kazi kwa manufaa maishani, na elimu ya dini.

“Awali, baada ya kuwafunza kucheza kandanda tulikuwa tunawaachilia kuenda nyumbani. Lakini baadaye tuliona haja ya kuhusisha mambo mengine kukuza maadili yao,” Bw Kamau aliambia Taifa Leo.

Mbali na kutoa mafunzo ya kabumbu, mkuu huyu anasimulia kwamba kituo hicho hutumia kandanda kama chambo cha kuvutia watoto kujumuika ili watiwe makali.

Tafa hukusudia kutimiza malengo yenye mihimili ya kutia fora katika elimu, uimarishaji talanta na kutoa ushauri wa masuala ya maisha.

“Wanafunzi wengi hapa huhudhuria masomo katika Shule ya Msingi ya Loldia. Kitambo, wengi hawakuenda shuleni lakini kupitia juhudi zetu, mahudhurio shuleni yameongezeka,” akaeleza Bw Kamau.

“Kaulimbiu yetu ya ‘kama huendi shule, huwezi kucheza kandanda’ imesaidia sana kuafikia madhumuni yetu,” akaongeza.

Pamoja na waanzilishi wengine, mkurugenzi huyu wa michezo alipoanza kituo hiki, watoto walihitajika kutoa angalau shilingi ishiriki kuwezesha ziara za michezo na kununua nyenzo tofauti zilizohitajika katika mazoezi ya kandanda.

“Tulianza kwa kushikana mkono hadi hatimaye mashirika kama vile shirika la utalii la Governor’s Camp na mengine yakaingilia kati,” Bw Kamau anasema.

Kadhalika, ili kuwavutia zaidi, watoto hawa hupewa uji kila siku kupitia msaada wa mashirika.

Mmoja wa wanajamii wanaojitolea kuwapa uji watoto na matineja wanaojiunga na Tafa. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Mimi hujitolea kuwaandalia uji watoto na wanarika wenzangu,” alisema Bi Eunice Kerubo ambaye amekamilisha kisomo cha sekondari maajuzi akisubiri kulipiwa karo ya chuo kikuu.

Bi Judith Akoth ni mmoja wa maafisa wa Tafa na majukumu yake ni kutoa mahamasisho kwa watoto wa kike.

Bi Judith Akoth, Kiongozi wa Maslahi ya Watoto wa Kike kituoni TAFA akijumuika na wasichana uwanjani. PICHA | LABAAN SHABAAN

Wengi wa watoto wa kike huishi katika jamii ya tabaka la chini katika mtaa wa Kasarani.

“Tangu kituo hiki kianzishwe, visa vya ujauzito wa utotoni vimepungua sana kupitia miradi yetu ya kukutana nao mara kwa mara kuwapa motisha,” alisema Bi Akoth.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UON), Frederick Otieno, amefadhiliwa na kituo hiki sababu ya usogora wake katika kandanda na kudumisha maadili bora.

“Nilianza kwa kujitolea hapa kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuwafunza watoto kompyuta na michezo ambapo nilibahatika kupata ufadhili kusoma UON,” akasema Bw Otieno.

Mwanafunzi wa UON Frederick Otieno aliyefadhiliwa na mashirika marafiki wa Talent Africa Football Academy Kasarani, Gilgil. PICHA | LABAAN SHABAAN

Baadhi ya wazazi walionufaika kwa watoto wao kusoma shule za upili wanasimulia jinsi ufadhili huu umewapunguzia mizigo ya malimbikizo ya karo yanayolemea mishahara yao midogo.

“Nimefurahi sana kwa sababu Tafa imenitoa mahali nisingejitoa. Sikuwahi kutarajia kama mtoto wangu atawahi kusoma shule ya sekondari,” akaungama Bi Elizabeth Afanda ambaye mtoto wake anasomeshwa katika shule ya upili ya St Andrew’s Tarambete, Gilgil.

Hapo mwanzo, ndoto yake Bw Kamau ilikuwa kama ya kukisiwa tu, lakini sasa inaakisiwa katika jitihada na maazimio ya watoto wanaochangamkia shughuli za kituo hiki kukwea vidato vya maisha.

“Kufikia sasa tumefadhili wanafunzi tisa kusoma katika shule za sekondari na katika vyuo vikuu. Mwaka 2024, tutawapeleka 16 katika shule za upili na sita katika vyuo vikuu,” alisema akifafanua kuwa wanaendelea kukagua ufaafu wa wanafunzi kuzingatia viwango vya uhitaji.

Bw Kamau anasifu kuwa akademia hii ya kandanda, imetuzwa kwa kushinda mashindano mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

Justina Syokau afunga mwaka na drama zake

Hatari ndani ya mabwawa ya kuogelea

T L