• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kanini Kega adai Raila na Kenyatta ndio walisababisha ashindwe kutetea kiti chake cha ubunge Kieni

Kanini Kega adai Raila na Kenyatta ndio walisababisha ashindwe kutetea kiti chake cha ubunge Kieni

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega amelaumu Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga akidai ndio walisababisha ashindwe kutetea kuhifadhi kiti chake cha ubunge Kieni Agosti 2022.

Kulingana na Katibu Mkuu huyo wa chama cha Jubilee, alisema Ijumaa, Julai 14, 2023 kwamba uamuzi wake kuunga mkono Bw Odinga kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 ndio ulimnyima fursa kurejea bungeni.

Bw Kega alimenyana na mbunge wa sasa Anthony Njoroge Wainaina, aliyeibuka mshindi kupitia tikiti ya chama cha UDA, kinachoongozwa na Rais William Ruto.

“Rais, ninakiri sikukupigia kura. Tulipanda mlima; Nilikuwa nasukuma yule mzee wa kitendawili (akimaanisha Raila Odinga). Nilikubali kushindwa, na ndio maana nilipata wadhifa EALA ambapo ninawakilisha nchi saba Afrika Mashariki,” Bw Kega akasema, akikashifu maandamano yanayoandaliwa na Odinga.

Mbunge huyo wa EALA ambaye ni Katibu Mkuu Jubilee alionya kuwa wanasiasa na wabunge wa chama hicho watakaoshiriki maandamano ya Azimio, wataadhibiwa kupitia sheria za chama.

“Kwa sababu hakubali kushindwa, kwa mujibu wa historia aliyoshiriki kuwania urais hatawahi shinda. Alikuwa na serikali – ‘deep state’, lakini akalemewa. Akubali alishindwa.”

Katika uchaguzi wa 2022, Raila Odinga (Azimio) alitoana kijasho na Rais wa sasa, Dkt Ruto aliyeibuka mshindi kupitia muungano wa Kenya Kwanza.

Kesi ya Azimio iliyowasilishwa katika Mahakama ya Juu zaidi nchini kupinga matokeo ya kura za urais, hata hivyo ilifutiliwa mbali na jopo la majaji lililoongozwa na Jaji Mkuu, CJ Martha Koome.

  • Tags

You can share this post!

Ruto asema hatakubali maandamano dhidi ya serikali ya KK

Maisha ya binadamu yana thamani kuliko maua, Sifuna...

T L