• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Kanu, Jubilee walaumiana kuhusu fujo

Kanu, Jubilee walaumiana kuhusu fujo

Na FLORAH KOECH

TOFAUTI kati ya madiwani wa vyama vya Jubilee na Kanu zinaendelea kudhihirika wazi katika Kaunti ya Baringo kutokana na ghasia zilizozuka Alhamisi jioni wakati wa kujadiliwa na kupigiwa kura ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Wakati wa kikao hicho, kaunti hiyo ilikuwa ya kwanza kuiangusha ripoti hiyo huku ubabe wa kisiasa kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi ukijitokeza miongoni mwa madiwani.Polisi walirusha vitoa machozi ndani ya bunge hilo baada ya upigaji kura na kuwalazimisha madiwani wakimbilie usalama wao.

Licha ya hali hiyo tete, Spika David Kiplagat ambaye aliongoza kikao hicho alitoa matokeo ya upigaji kura na kutamatisha vikao hivyo kisha kutangaza kuwa vikao hivyo vitarejelewa Jummanne wiki ijayo.

Madiwani wanaoegemea mrengo wa Jubilee walipig kura ya kupinga mswada huo huku 11 wa Kanu na vyama vingine wakiunga mkono.

Hata hivyo, madiwani wa Kanu sasa wanadai mswada huo ulijadiliwa na kupitishwa kiharamu kwa kuwa maoni ya umma hayakupokelewa.

Diwani maalumu Betty Birchogo alimshutumu Spika kwa mapendeleo na kukosa kuhakikisha sheria inafuatwa wakati wa mjadala.

“Walikuwa wakiharakisha mswada huo ili kuwafurahisha wakuu wao wa kisiasa ambao wamekuwa wakizunguka taifa wakipinga BBI,” akasema Bi Birchogo.

“Inasikitisha Spika alikuwa na mapendeleo na alikataa kusikiliza malalamishi yetu kisha akaendelea kuwasilisha mswada wenyewe,” akaongeza.

Diwani wa Churo/Amaya Ameja Selemoi alidai kikao hicho kiliharakishwa ilhali kulikuwa na hoja zilizofaa kujadiliwa kabla ya mswada huo kuwasilishwa.

Lakini madiwani wa Jubilee wamemshutumu Seneta Gideon Moi kwa kuhusika na ghasia zilizotokea katika bunge hilo.

Diwani wa wadi ya Mochongoi, Kipruto Kimasop alitetea kuangushwa kwa BBI, akisema walitoa notisi kuhusu kujadiliwa na kupigiwa kura mswada huo jukumu lililotekelezwa na Mwenyekiti wa kamati ya sheria Charles Kosgei.

“Madai kwamba mchakato huo haukufuata sheria hayana mashiko. Mswada huo ulijadiliwa na ushahidi upo,” akasema Bw Kimosop.

  • Tags

You can share this post!

Matatu iliyoua abiria 9 ilikiuka kanuni za kudhibiti...

Ratiba ya mazishi ya Nyachae yabadilishwa