• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Karim Benzema anyakua taji la Ballon d’Or kwa mara ya kwanza

Karim Benzema anyakua taji la Ballon d’Or kwa mara ya kwanza

Na MASHIRIKA

FOWADI mzoefu wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Karim Benzema, ndiye mshindi wa taji la Ballon d’Or ambalo hutolewa kwa mchezaji bora zaidi duniani.

Benzema ambaye ametwaa taji hilo kwa mara ya kwanza kabisa, alifunga mabao 44 katika mechi 46 na kusaidia waajiri wake Real kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kuzoa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021-22.

Lionel Messi (mara saba) na Cristiano Ronaldo (mara tano) walikuwa wakijivunia kunyanyua taji la Ballon d’Or mara 12 katika makala 13 ya awali.

Mfumaji matata wa Bayern Munich, Sadio Mane, aliyekuwa kambini mwa Liverpool mnamo 2021-22, aliambulia nafasi ya pili nyuma ya kiungo mahiri wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin de Bruyne.

Alexia Putellas wa Barcelona alifaulu kuhifadhi taji la Ballon d’Or kwa upande wa wanawake mnamo 2022. Fowadi wa Arsenal, Beth Mead aliyesaidia Uingereza kunyakua taji la Euro 2022, aliridhika na nafasi ya pili.

Klabu ya Manchester City inayonogesha soka ya EPL ilikuwa na wawaniaji sita wa taji la Ballon d’Or mwaka huu. Kikosi hicho kilitwaa taji la Klabu Bora baada ya kupiku Liverpool.

Taji la Ballon d’Or mwaka huu ilitolewa kwa mchezaji bora ambaye matokeo yake yaliridhisha zaidi katika msimu wa 2021-22.

Benzema ndiye Mfaransa wa kwanza kushinda taji la Ballon d’Or baada ya Zinedine Zidane mnamo 1998. Zidane alihudhuria hafla ya kutawazwa kwa Benzema mnamo Jumatatu usiku jijini Paris na ndiye alimtuza Mfaransa mwenzake.

Kati ya mabao 44 ya Benzema, matatu yalikuwa katika pambano moja la UEFA lililomshuhudia akicheka na nyavu chini ya dakika 17 za kipindi cha pili dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG). Alifunga mabao mengine matatu dhidi ya Chelsea ugenini kwenye mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya UEFA.

Benzema, 34, alifunga mabao mengine matatu zaidi katika mikondo miwili ya michuano miwili ya nusu-fainali za UEFA dhidi ya Man-City.

Nyota huyo ambaye amekuwa akichezea Real tangy 2009, anatarajiwa kuwa tegemeo kubwa la Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kuanzia Novemba 20, 2022.

Mshindi wa Ballon d’Or huamuliwa na kura za wanahabari 100 kutoka kote duniani.

Thibaut Courtois wa Real alitwaa taji la Yashin Trophy ambalo hutolewa kwa Kipa Bora zaidi duniani. Alisson Becker wa Liverpool aliambulia nafasi ya pili huku Ederson (Man-City) na Edouard Mendy (Chelsea) wakiridhika na nafasi za tatu na nne mtawalia. Hugo Lloris wa Tottenham Hotspur alimaliza wa 10.

Taji la Kopa Trophy ambalo hutolewa kwa Chipukizi Bora wa chini ya umri wa miaka 21 lilimwendea tineja wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Gavi, ambaye alifikisha umri wa miaka 18 mnamo Agosti.

Kiungo wa Borussia Dortmund, Jude Bellingham, 19, aliambulia nafasi ya nne huku mwenzake katika timu ya taifa ya Uingereza, Bukayo Saka, 21, akitupwa nafasi ya nane.

Robert Lewandowski wa Barcelona alitwaa taji la Gerd Muller Trophy ambalo hutolewa kwa Mshambuliaji Bora zaidi. Nyota huyo wa Ujerumani alifungia Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland mabao 57 mnamo 2021-22.

Tuzo ya Socrates Award ambalo hutolewa kwa mwanasoka karimu zaidi lilitwaliwa na Mane ambaye anafanya kazi nyingi ya hisani nchini Senegal.

Messi na Ronaldo wametamalaki tuzo ya Ballon d’Or katika miaka ya hivi karibuni isipokuwa 2018 ambapo taji hilo lilitwaliwa na kiungo matata wa Real na timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric.

Straika wa Manchester United, Mreno Cristiano Ronaldo wakati wa mechi yao ya UEFA Europa katika Kundi E ambapo Omonia Nicosia ilikaribisha Manchester United katika uwanja wa GSP jijini Nicosia mnamo Oktoba 6, 2022. PICHA | AFP

Messi alijishindia taji hilo mnamo 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021. Hata hivyo, hakuteuliwa kabisa kuwania taji hilo mwaka huu kutokana na matokeo dunia katika msimu wake wa kwanza kambini mwa PSG.

Ronaldo wa Manchester United alijizolea taji la Ballon d’Or kwa mara ya mwisho mnamo 2017 na aliambulia nambari 20 mwaka huu kwenye orodha ya wanasoka 30. Hiyo ndiyo nafasi ya chini zaidi kwa nyota huyo raia wa Ureno kuwahi kushikilia kwenye tuzo hiyo tangu 2005.

Orodha ya Ballon d’Or:

  1. Karim Benzema (Real Madrid, Ufaransa).
  2. Sadio Mane (Bayern Munich, Senegal).
  3. Kevin de Bruyne (Manchester City, Ubelgiji).
  4. Robert Lewandowski (Barcelona, Poland).
  5. Mohamed Salah (Liverpool, Misri).
  6. Kylian Mbappe (Paris St-Germain, Ufaransa).
  7. Thibaut Courtois (Real Madrid, Ubelgiji).
  8. Vinicius Junior (Real Madrid, Brazil).
  9. Luka Modric (Real Madrid, Croatia).
  10. Erling Haaland (Manchester City, Norway).
  11. Son Heung-min (Tottenham Hotspur, Korea Kusini)
  12. Riyad Mahrez (Manchester City, Algeria).
  13. Sebastien Haller (Borussia Dortmund, Ivory Coast).
  14. Fabinho (Liverpool, Brazil) alikamata nafasi moja na Rafael Leao (AC Milan, Ureno).
  15. Virgil van Dijk (Liverpool, Uholanzi).
  16. Luis Diaz (Liverpool, Colombia) alikamata nafasi moja na Dusan Vlahovic (Juventus, Serbia) na Carlos Casemiro (Manchester United, Brazil).
  17. Cristiano Ronaldo (Manchester United, Ureno).
  18. Harry Kane (Tottenham Hotspur, Uingereza).
  19. Trent Alexander-Arnold (Liverpool, England) alikamata nafasi moja na Phil Foden (Manchester City, England) na Bernardo Silva (Manchester City, Ureno).
  20. Joao Cancelo (Manchester City, Ureno) alikamata nafasi moja na Joshua Kimmich (Bayern Munich, Ujerumani), Mike Maignan (AC Milan, Ufaransa), Antonio Rudiger (Real Madrid, Ujerumani), Darwin Nunez (Liverpool, Uruguay) na Christopher Nkunku (RB Leipzig, Ufaransa).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Faida za mboga aina ya karela (bitter gourd)

LISHE: Vyakula vigumu kusagika mwilini

T L