• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Karua aahidi ‘kuwakomboa’ wakazi Mlimani

Karua aahidi ‘kuwakomboa’ wakazi Mlimani

NA WANDERI KAMAU

MGOMBEA mwenza wa mwaniaji urais wa Azimio La Umoja-One Kenya, Raila Odinga, Bi Martha Karua, Ijumaa alisema kuwa serikali ya Azimio “itawaokoa” wenyeji wa Mlima Kenya kutokana na changamoto zinazowakabili katika masuala ya biashara na sekta ya kilimo.

Bi Karua alisema kwamba kama mwenyeji wa eneo hilo, anafahamu changamoto ambazo wenyeji wamekuwa wakipitia katika sekta ya biashara, hasa kwenye uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio na televisheni vinavyotangaza kwa lugha ya Kikuyu, Bi Karua alisema mojawapo ya masuala watakayoyapa kipaombele ni kubuni mazingira mwafaka ya kibiashara kwa wafanyabiashara wa hapa nchini na wawekezaji kutoka nje.

Wafanyabiashara wengi katika eneo hilo wamekuwa wakilalamikia mazingira magumu ya kufanyia biashara tangu janga la virusi vya corona kutokea nchini mnamo 2020.

“Hatutampendelea yeyote. Tutatoa nafasi sawa kwa wafanyabiashara wetu na wale kutoka nje kwani tutawategemea wote kuistawisha nchi kupitia ushuru watakaolipa,” akasema Bi Karua.

Vile vile, aliahidi kurahisisha mfumo wa utoaji leseni kwa wafanyabiashara na kulainisha utendakazi wa Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA).

Alisema serikali ya kitaifa itashirikiana na zile za kaunti kuunganisha taratibu za utoaji leseni kwa wafanyabiashara, ili kuondoa hali ambapo baadhi yao hutozwa ada tofauti na serikali zote mbili kwa huduma sawa wanazotoa.

Kuhusu utendakazi wa KRA, alisema watabuni mkakati mpya, ambapo halmashauri hiyo itaanza kuwachukulia wafanyabiashara kama washirika wake, wala si maadui wake.

“Huenda kubadilisha jina la KRA kukakosa kuzaa matunda ikiwa utendakazi wake hautalainishwa. Tutabadilisha mfumo wake wa utoaji huduma ili kuhakikisha hakuna mwekezaji ama mfanyabiashara yeyote anayehangaishwa bila kosa lolote. Badala yake, iitawaadhibu tu wale watakaokosa kulipa ushuru kama inavyotakikana,” akasema Bi Karua.

Kauli yake ilionekana kuchangiwa na mvutano ambao umekuwepo kati ya halmashauri hiyo na kampuni ya kutengeneza vileo ya Keroche, ambapo KRA imekuwa ikiilaumu kwa kukwepa kulipa zaidi ya Sh300 milioni kama ushuru.

Alhamisi, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Bi Tabitha Karanja, alipata afueni, baada ya Mahakama Kuu kuiagiza KRA kuifungua upya kampuni, iliyo katika eneo la Naivasha, Kaunti ya Nakuru.

Ikizingatiwa eneo hilo limekuwa likikabiliwa na tatizo la matumizi ya mihadarati, hasa miongoni mwa vijana, Bi Karua alitangaza mpango wa muungano huo kubuni vituo vya kurekebishia tabia, ili kuwasaidia vijana waliozidiwa na uraibu wa mihadarati.

Alisema vituo hivyo vitatumika kuwasaidia vijana kurejelea shughuli za ujenzi wa taifa, kinyume na sasa ambapo wengi wao wanaonekana kupoteza mwelekeo maishani kutokana na ulevi.

Kauli ya Bw Karua inajiri wiki moja baada ya kushiriki kwenye Mdahalo wa Wawaniaji Wenza wa Urais uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), Nairobi, Jumanne iliyopita.

  • Tags

You can share this post!

Sonko sasa aunga Omar wa UDA kuwa gavana

Raila alaani fujo huku wafuasi wa wagombeaji ugavana...

T L