• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Kidero aahidi kuonyesha ODM kivumbi akisaka ugavana Homa Bay

Kidero aahidi kuonyesha ODM kivumbi akisaka ugavana Homa Bay

NA GEORGE ODIWUOR

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero wikendi alianzisha rasmi kampeni za kusaka kiti cha ugavana wa Kaunti ya Homa Bay kama mwaniaji huru baada ya kujiondoa ODM.

Dkt Kidero alijiondoa katika chama hicho wiki jana, baada ya viongozi wa ODM kukutana na kinara wao Raila Odinga Nairobi na kuafikiana kuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike Gladys Wanga, apokezwe tikiti ya moja kwa moja.

Kinaya ni kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi wa ODM, Bi Catherine Mumma kwenye mahojiano na kituo kimoja kinachotangaza kwa Kijaluo Jumanne wiki iliyopita, alisema chama kitatoa tikiti ya moja kwa moja maeneo ambapo kuna mwaniaji mmoja pekee.

Dkt Kidero, hata hivyo, alisema haogopi wala hatajiondoa kwenye kiny’ang’anyiro hicho, huku akisema yupo tayari kupambana na Bi Wanga debeni.

“Tikiti ya moja kwa moja hutolewa tu pale ambapo viongozi huwa wamekubaliana kuwa mwaniaji awe mtu fulani. Kuhusu uamuzi wa ODM, mimi na mwaniaji mwengine hatukualikwa kwenye mkutano huo na mimi nitafika debeni kwa sababu nina maono ya kubadilisha uongozi wa kaunti hii,” akasema Dkt Kidero.

“Nitaendelea na kampeni zangu hadi tamati na nina matumaini kuwa nitashinda kiti hiki cha ugavana kutokana na yale yaliyoko kwenye ajenda na manifesto yangu,” akaongeza.

Dkt Kidero na mfanyabiashara Luis Ogingo, ambaye pia alikuwa akiotea tikiti ya ODM, hawakuhudhuria mkutano wa Nairobi na wote wamekataa uamuzi wa kumpa Bi Wanga tikiti ya moja kwa moja.

Wakati wa mkutano huo, aliyekuwa mbunge wa Kasipul, Bw Oyugi Magwanga, aliteuliwa kama mgombeaji mwenza wa Bi Wanga. Wengine waliojiondoa kiny’ang’anyironi ili kumuunga mkono Bi Wanga ni Mwenyekiti wa ODM John Mbadi, Katibu wa Kaunti ya Homa Bay Isaiah Ogwe, Naibu Gavana Hamilton Orata na Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai Akelo Misori.

Akihutubia misururu ya mikutano ya kampeni katika kijiji chake cha Wikoteng’ eneobunge la Rangwe, Dkt Kidero alisema uamuzi wake wa kugura ODM hakufai kufasiriwa kuwa yupo kwenye vita vya kisiasa na Bw Odinga.

Dkt Kidero pia alimwonya Gavana Cyprian Awiti asiingilie siasa za urithi akimkashifu kwa kutofanya maendeleo yoyote ya maana kusaidia kaunti hiyo kunufaikia ugatuzi tangu 2013.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Bahili akausha boda na kuipapia probox

Katibu mkuu ashtakiwa kumzaba mkewe makonde akiwa na mimba

T L