• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
KILIMO NA BIASHARA: Anavuna hadi Sh800,000 kwa mwezi kupitia zao la kungumanga

KILIMO NA BIASHARA: Anavuna hadi Sh800,000 kwa mwezi kupitia zao la kungumanga

Na BENSON MATHEKA

KWA wengi, mkungumanga ni mmea usio na faida lakini sio kwa Velji Senghani, 62, anayevuna mamilioni kutoka kwa mmea huu.

Alianza kilimo cha kungumanga Pomegranet mwaka 1989 eneo la Masinga kaunti ya Machakos.

Awali alikuwa mkandarasi wa mijengo jijini Nairobi.

“Niliacha kazi hiyo na kuamua kuendeleza kilimo,” asema Senghani ambaye ni raia wa India na Kenya.

Na faida yake kutoka kilimo cha kungumanga ni zaidi ya Sh800,000 kwa mwezi.

Anasema alichagua eneo la Masinga, Kaunti ya Machakos kwa sababu kuna hali ya hewa sawa na India.

“Najivunia sana kuwa Ukambani kwa sababu hali ya hewa ni sawa na India. Sikupenda kwenda sehemu zenye baridi bali niliamua kuishi Ukambani kwa sababu kuna utulivu, mashamba ni makubwa kwa kilimo. Matunda kama kungumanga hufanya vizuri sana sehemu hii na mchanga ni wenye rotuba nzuri,” asema Senghani.

Maembe, machungwa

Mbali na kuwa mkulima wa kungumanga eneo hili, Senghani amekumbatia sana ukulima wa maembe, machungwa na pilipili hoho.

“Niliamua kuuza shamba langu huko India na nikafanya mpango wa kununua shamba hapa Kenya. Nina shamba la ekari 12 nililonunua na ekari 25 za kukodi,” aeleza.

Anasema alipenda kilimo tangu utotoni lakini hakubahatika kusomea taaluma hii lakini alikutana na wakulima waliobobea sana waliompa ushauri na akaajiri baadhi yao.

“Niliponunua shamba sikupenda kukaa bure kwa sababu nilijua nina familia. Nina mke na wavulana wawili, mmoja anaendeleza kazi ya ujenzi baada yangu kustaafu na yule mwingine ananisaidia hapa nyumbani kusafirisha matunda kwa lori kwenda kuyauzia wateja wangu,” aeleza Senghani ambaye ameishi Kenya kwa miaka 30 sasa.

Anasema ukulima wa kungumanga pamoja na matunda mengine anayopanda umemletea faida nyingi kila mwaka.

“Kungumanga huzaa kila wakati kama unanyunyuzia maji na dawa inayofaa.Kungumanga huuzwa kati ya Sh100 na Sh200 kwa kilo kulingana na misimu. Kungumanga si rahisi kupanda na kukuza kwa sababu inahitaji maji kwa wingi lakini ukitunza mmea huu vizuri utapata faida nyingi,” aeleza. Ili kupata maji alichimba visima katika shamba lake.

“Kwa upande wa machungwa huwa nauza kilo moja kati ya Sh80 na Sh120 kulingana na msimu. Bei ya maembe kilo moja ni kati ya Sh50 na Sh100 kulingana na misimu pia,” asema Senghani. Mkulima huyu anasema kuna njia ya kufanikiwa katika ukulima wa matunda haya.

“Biashara yoyote si rahisi lakini ukiwa na uvumilivu unaweza kufanikiwa pakubwa sana. Kwanza lazima utafute wafanyakazi ambao watakusaidia kufanya kazi, utayarishe shamba lako vizuri, utafute dawa na mbolea inayofaa mimea yako,” aeleza.

Katika ukulima alipatana na mshauri wa wakulima Abraham Mutuku ambaye ndiye aliyempa ushauri na akafanya kazi katika shamba lake hadi sasa kwa sababu alikuwa amebobea sana katika kukuza matunda na mimea mingine.

Anasema baada ya kupanda mimea ya matunda huanza kuvuna baada ya miaka mitatu unusu.

“Kila mwaka huwa ninapata mavuno mazuri. Kwa mwezi huwa ninapata faida isiyopungua Sh800,000 baada ya kuuza kungumanga, machungwa na maembe. Huvuna maembe mara moja kwa mwaka lakini kungumanga na machungwa huvuma misimu mingi kwa mwaka,” asema Senghani.

Anasema wateja wake hujivunia sana kwa sababu anawauzia mavuno mazuri na ambayo ni safi.

“Wateja wangu ni wa kawaida na wa kampuni. Huwa ninauza matunda yangu kwa kampuni ya Fresh n’ Juicy Nairobi ambayo hutengeneza sharubati na kuuzia maduka ya Nakumatt na supermarket zingine. Nakuza machungwa aina ya Voi Pix, Washington Dover na Sadra. Maembe nakuza aina ya Kent,” asema Senghani.

Licha ya mkulima huyu kufanikiwa pakubwa katika ukulima, amekumbana na changamoto si haba.

“Kwanza nilipoamua kuanzisha ukulima huu nilijua kuna shida ya maji. Watu wengi eneo hili wanategemea mvua pekee kwa sababu hakuna mito yenye maji ya kutosha. Hata hivyo, nilichimba kisima ambacho kilinigharimu zaidi ya Sh800,000. Kwa sasa sina shida ya maji ya kunyunyuzia mimea yangu,” aeleza.

“Kuna magonjwa ya mimea ambayo hutumia gharama nyingi ya kununua dawa. Kuna ndege hudona matunda na kuyaharibu, wafanyakazi wakati mwingi hukosekana na hali hiyo inafanya kukadiria hasara, wadudu waharibifu na mvua ikiwa nyingi wakati huharibu matunda,” asema Senghani.

Anashauri watu kukumbatia ukulima wa matunda. “Ninasihi watu wajitume kabisa kupanda mimea ya matunda. Nina uwezo wa kuwatafutia soko wakiniuzia matunda yao. Watumie mashamba vizuri kwa kupanda licha ya changamoto wanazopitia. Pia nawapa fursa ya kutembelea shamba langu na kuona kazi ambayo nimefanya na waelimike,” asema Senghani.

You can share this post!

Wakazi Laikipia Kaskazini walia wawekezaji, wakulima...

AKILIMALI: Ujuzi wa kupanga maua nyumba za kifahari wamuinua

adminleo