• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Kinyesi cha binadamu chatumika kuzuia MCAs kumbandua gavana wa Nyamira

Kinyesi cha binadamu chatumika kuzuia MCAs kumbandua gavana wa Nyamira

NA WYCLIFFE NYABERI 

KINYESI cha binadamu na mawe lori nzima Jumanne asubuhi, Septemba 26, 2023 vilipatikana vimemwagwa nje ya lango la kuingia Bunge la Kaunti ya Nyamira mswada unaolenga kumng’atua afisini Gavana Amos Nyaribo ukitarajiwa kuwasilishwa.

Madiwani (MCAs) wa Nyamira wametishia kumbandua gavana wa kaunti, kwa msingi kuwa anatumia vibaya mamlaka yake na ofisi.

Vizuizi hivyo vililetwa usiku wa manane, kuamkia Jumanne, na watu wasiojulikana kama njia mojawapo kutatiza kuwasilishwa kwa mswada huo.

Maafisa wa polisi wakishirikiana na wale wa kutekeleza amri za kaunti wameshika doria kwenye lango kuu wakikagua kwa makini kila anayeingia bungeni.

MCAs 28 kati ya 34 wa kaunti hiyo tayari wameonyesha kutokuwa na imani na gavana Nyaribo na wako radhi kumbandua kwa kile wanasema anatumia afisi yake visivyo.

Mzozo kati ya madiwani na Gavana Nyaribo ulitokota pale kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) alimfuta kazi Waziri wake wa Afya Timothy Ombati.

Bw Nyaribo alisema Ombati alikuwa amehusika kwenye ufujaji wa pesa zilizohitajika kwenye ununuzi wa dawa hospitalini.

Alidai waziri huyo alimhadaa kwa kuzindua maboksi tupu ambayo hayakuwa na dawa.

Hata hivyo, Bw Ombati alikana madai hayo, baadhi ya madiwani wakimtetea wakisema alikuwa mwathiriwa tu wa sakata kubwa ya ufisadi inayoandama Gavana Nyaribo.

Jana, Jumatatu kiranja wa wengi bunge la kitaifa, Bw Silvanus Osoro alikutana na madiwani hao na kuwasihi watatue mzozo wao kiustaarabu lakini wakamweleza kwamba hawatalegeza kamba.

Pia gavana Nyaribo amekuwa akiwasihi MCAs hao wajadiliane kuondoa uasi baina yao lakini mikakati yake haijafua dafu.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Raha ya watahiniwa wa KCSE 2023 masomo ya lazima...

Serikali kuharibu pasipoti 10,000 za waliozembea kuzichukua

T L