• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Kipchoge afagia NN Marathon, macho sasa kwa Olimpiki

Kipchoge afagia NN Marathon, macho sasa kwa Olimpiki

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge, alirejea kunogesha fani hiyo kwa matao ya juu hapo Jumapili na kuibuka mshindi wa NN Mission Marathon mjini Enschede, Twente, Uholanzi.

Kipchoge alikata utepe baada ya muda wa saa 2:04:30 mbele ya Mkenya mwenzake Jonathan Korir aliyesajili muda bora wa saa 2:06:40. Kipchoge alipokezwa bendera ya Kenya na kocha wake Patrick Sang aliyekuwa akimsubiri mwishoni mwa mbio hizo.

Goitom Kifle wa Eritrea aliridhika na nafasi ya tatu (2:08:07) mbele ya Stephen Kiprotich wa Uganda (2:09:04) aliyefunga orodha ya nne-bora.

Mkenya mwingine aliyetia fora kwenye kivumbi hicho ni Mathew Sang aliyekamata nafasi ya sita (2:09:54), nyuma ya Geoffrey Kusuro wa Uganda (2:09:53). Ingawa Mkenya Philemon Kacheran alikamilisha mbio hizo katika nafasi ya nne (2:08:45), matokeo yake hayakutambuliwa rasmi kwa kuwa alikuwa miongoni mwa watimkaji waliokuwa wakiwawekea kasi washindani wengine.

Gladys Chesir aliyekuwa mwakilishi wa pekee wa Kenya kwa upande wa wanawake, aliambulia nafasi ya nane kwa muda wa saa 2:29:16.

Kitengo hicho cha wanawake kilitawaliwa na Katharina Steinrueck kutoka Ujerumani (2:25:59). Sara Moreira wa Ureno alikamata nafasi ya pili (2:26:42) mbele ya Wajerumani Rabea Schoeneborn (2:27:03) na Laura Hottenrott (2:28:02) walioridhika na nafasi za tatu na nne mtawalia.

Mbio za NN Mission Marathon zilikuwa za kwanza kwa Kipchoge kushiriki tangu Oktoba 2020 ambapo alitupwa hadi nafasi ya nane kwenye London Marathon, Uingereza.

Noah Kipkemboi aliyekuwa pia akimtia kasi Kipchoge, aliondoka ulingoni baada ya hatua ya kilomita 25. Kipchoge aliongoza kundi la kwanza katika mbio hizo hadi kilomita 33 alipochomoka na kumwacha Korir. Alidumisha kasi yake hadi hatua ya kilomita 40 aliyoifikia baada ya saa 1:57:58.

“Hiki kilikuwa kipimo halisi cha maandalizi yangu. Ninafurahi kwamba nilikimbia vizuri na kukamilisha mbio hizo kwa muda ambao nimeridhishwa nao,” akatanguliza Kipchoge.

“Waandalizi walifanya kazi nzuri na kwa sasa napanga kurejea Kenya kuimarisha zaidi maandalizi yangu kwa ajili ya Olimpiki zijazo za Tokyo, Japan,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba atakuwa katika mashuariano ya mara kwa mara na wasimamizi wake pamoja na vinara wa Team Kenya.

“Hali ya hewa ilikuwa shwari japo kulikuwa na upepo mkali ulionipunguzia kasi. Hata hivyo, nisingependa kulalamikia sana hali ya hewa kwa sababu ilituathiri sote tuliokuwa washiriki wa mbio hizo,” akaongeza.

Kivumbi hicho kilivutia zaidi ya wanariadha 50 kutoka mataifa mbalimbali waliokuwa wakilenga kusajili muda wa kufuzu kwa michezo ijayo ya Olimpiki itakayoandaliwa nchini Japan kati ya Julai na Agosti 2021.

Washiriki wa NN Mission Marathon walilazimika kupiga mizunguko minane uwanjani Twente Airport ila mashabiki hawakuruhusiwa kuhudhuria kivumbi hicho kutokana na janga la corona.

Awali, mbio hizo zilikuwa zimeratibiwa kufanyika mjini Hamburg, Ujerumani mnamo Aprili 11 ila zikaahirishwa kwa kipindi cha wiki moja na kuhamishiwa nchini Uholanzi kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani.

Kipchoge kwa sasa atakuwa akipania kuwa mwanariadha wa tatu wa kiume kutetea nishani ya dhahabu kwenye Olimpiki mnamo Agosti.

Abebe Bikila wa Ethiopia (1960 Roma, 1964 Tokyo) na Mjerumani Waldemar Cierpinski (1976 Montreal, 1980 Moscow) ndio wanariadhwa wawili wa pekee waliowahi kutetea ufalme wao katika mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki.

You can share this post!

Kafyu ya unyama

Al Duhail yatoka sare na Al Ahli Saudi kwenye Klabu Bingwa...