• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
Kiptum ahifadhi la taji la mbio za viziwi nusu marathon

Kiptum ahifadhi la taji la mbio za viziwi nusu marathon

Na JOHN KIMWERE

DANIEL Kiptum kutoka Nandi alijituma mithili ya mchwa na kufanikiwa kuhifadhi ubingwa wa mbio za viziwi za nusu marathon (kilomita 21) makala ya sita kitengo cha wanaume zilizofanyika mjini Kericho.

Kiptum mshindi wa dhahabu kwenye mbio za Sumsun Deafly Games 2017 nchini Uturuki alitwaa taji hilo baada ya kutimka muda wa saa 1:11.16 na kumpiku Lucas Wandia aliyemaliza kwa muda wa saa 1:11.58. Naye David Njeru alimaliza kwa muda wa saa 1:12.00 na kuibuka tatu bora.

Mashindano hayo huandaliwa na kufadhiliwa na kampuni ya simu za rununu ya Safaricom na kuleta pamoja washiriki kutoka maeneo tofauti nchini kuonyesha talanta zao.

Kitengo cha wanawake, Juster Moraa Kwamesa alihifadhi taji hilo alipotimka muda wa saa 1:42.01. Alifuatiwa kwa karibu na Priscah Naibin (1:42.09) na Rebeca Matiko (1:55.5) waliomaliza nafasi ya pili na tatu mtawalia.

”Nina furaha tele kuhifadhi taji hilo ingawa haikuwa rahisi. Ninalenga kuzamia mazoezi zaidi kujinolea riadha za Afrika zitakazofanyika Septemba 1, mwaka huu katika Uwanja wa Moi Sports Centre, Kasarani Nairobi,” Daniel Kiptum alisema.

Daniel Kiptum akimaliza wa kwanza kwenye mbio za viziwi za kilomita 21 makala ya sita alipohitaji taji hilo aliloshinda mwaka jana kitengo cha wanaume. Picha/ John Kimwere

Mbio za kilomita kumi, Geoffrey Kamia na Jentrix Dindi walitawazwa mabingwa kwa wanaume na wanawake mtawalia baada ya kutimika dakika 36:00 na 47:46.

Naye Gilbert Kirui (36:02) na Dennis Kiprop (37:00) walimaliza nafasi ya pili na tatu mtawalia kitengo cha wanaume. Kwa wanawake, Mercy Moraa na Viola Jelimo walitawazwa washindi wa nafasi ya pili na tatu baada ya kutimka muda wa dakika (47:50) na (48:18) mtawalia.

Mabingwa wa Half Marathon walituzwa kitita cha Sh100,000 kila mmoja upande wa wanaume na wanawake.

Nao waliomaliza nafasi ya pili na tatu walipokea Sh50,000 na Sh30,000 mtawalia. Washindi kwenye mbio za kilomita kumi walitia kibindoni Sh50,000 kila mmoja.

”Tulikuwa na wakati mzuri katika mashindano ya makala ya mwaka huu. Ningependa kutangaza kuwa waliibuka kati ya tatu bora katika mbio za half marathon na kilomita kumi wameshajikatia tikiti ya kushiriki riadha za Afrika mwaka huu,” katibu wa muungano wa wanariadha viziwi (DAAK), Bernard Banja alisema.

Mashindano ya makala ya mwaka huu yalidhaliwa kwa kitita cha Sh2.5 milioni.

You can share this post!

Kahawa Queens wazidi kudhihirisha makali yao

Luis Garcia kuhudhuria fainali za Chapa Dimba

adminleo