• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Kiti balozi kinachofundisha ubunifu, kupigana na taka za plastiki

Kiti balozi kinachofundisha ubunifu, kupigana na taka za plastiki

NA KALUME KAZUNGU

KAUNTI ya Lamu imekuwa ikigonga vichwa vya habari Kenya na ulimwengu mzima kupitia ubunifu mbalimbali.

Miongoni mwa ubunifu huo ni ule wa mashua ya kwanza na ya kipekee kuwahi kutengenezwa ulimwenguni kupitia taka za plastiki zilizokusanywa kutoka fukwe mbalimbali za Bahari Hindi eneo hilo.

Mashua hiyo ilitengenezwa kupitia mradi kwa jina Flip Flopi, chini ya mzinduzi wake mkuu na mzawa wa Lamu Ali Skanda.

Mashua hiyo ya Flip Flopi ilijizolea umaarufu mkubwa duniani, hatua iliyopelekea chombo hicho kufanywa kielelezo na uwajibikaji kwa wahifadhi wa mazingira.

Punde ilipozinduliwa, mashua hiyo ya taka za plastiki ilizungushwa nchi mbalimbali na ulimwenguni kuhamasisha watu na wadau tofauti tofauti kuhusu umuhimu wa kuyatunza mazingira yasiharibiwe kupitia utumiaji na utupaji ovyo wa plastiki, iwe ni baharini au nchi kavu.

Wakati ulimwengu ukiendelea kustaajabishwa na ubunifu huo wa mashua ya taka za plastiki, shirika la Flip Flopi limezinduka tena na mapya mengine ya kuunda kiti maalumu kupitia taka za plastiki zilizokusanywa baharini na nchi kavu na jamii za Lamu.

Kiti hicho cha aina yake siku za hivi karibuni kimegeuzwa kuwa balozi kufundisha, iwe ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari au wanagenzi wa taasisi na vyuo mbalimbali nchini kuhusu ubunifu na umuhimu wake na pia kupigana na changamoto ya taka za plastiki Lamu, nchini na ulimwengu mzima.

Kiti hicho kimekuwa kikianikwa wazi au kutandazwa wakati wa hafla mbalimbali za elimu, kijamii, kitaifa na hata kimataifa, dhamira kuu ikiwa ni kuwahamasisha waja kuhusiana na umuhimu wa kuwa wabunifu maishani ili kuwawezesha kusuluhisha matatizo ya kimsingi wanayokumbana nayo kwenye mazingira wanamoishi kila siku.

Katika kaunti ya Lamu, utapata kiti hicho kikionyeshwa mbele ya hadhira wakati wa sherehe za mahafali vyuoni, kwenye makongamano ya kujadili mazingira na mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa shughuli nyingine.

Wakati wa ziara ya Mfalme Charles wa Uingereza humu nchini mwaka 2023, wakuu wa Flip Flopi wakiongozwa na Bw Skanda walijitokeza na kumzawadia mfalme huyo kiti cha taka za plastiki walichokitengeneza kwa muundo wa kifalme.

Wakati wa hafla ya mahafali kwenye chuo cha kiufundi cha mjini Lamu hivi majuzi, wakuu wa Flip Flopi pia waliwasilisha kiti kilichotengenezwa kwa taka za plastiki, ambapo waliwahamasisha mahafali kuibukia ubunifu maishani wanapokuwa masomoni na hata wanapohitimu na kutoka nje na vyeti, shahada au stashahada zao, hivyo kuepuka kujikalia bure bila shughuli.

Ni wakati wa hafla hiyo, ambapo pia wakuu wa Flip Flopi wakiongozwa na Bw Skanda walimtunuka Gavana wa Lamu Issa Timamy kiti cha taka za plastiki ili kuweka na kukitumia kiti hicho afisini mwake, hivyo kuendeleza hamasa au kupitisha ujumbe kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kuwashinikiza watu kuwa wabunifu katika jamii.

Kiti Balozi kikiwa mbele ya Gavana wa Lamu Issa Timamy akiwa na baadhi ya wanafunzi na watu wengine. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Alhamisi, Bw Skanda alisema ni kupitia ubunifu wao ambapo wamefaulu kupitisha vyema hamasa na maonyo kuhusu watu, hasa wale wanaoishi Pwani au kupakana na maji makuu, ikiwemo Bahari Hindi, maziwa nakadhalika dhidi ya uchafuzi wa mazingira.

“Azma kuu ya kuibuka na ubunifu huu ni kupitisha ujumbe kwa watu kuepuka matumizi ya plastiki ambazo zimedhihirisha wazi kuwa na athari chungu nzima kwa mazingira yetu, iwe ni yale ya baharini au nchi kavu. Isitoshe, maarifa yetu ya kutengeneza viti au mashua kupitia taka za plastiki pia inaleta mhemko kwa wanafunzi kuibukia sana ubunifu kwenye masomo kabla, wakati na hata baada ya kuhitimu kwao ili waweze kuajiriwa au kujiajiri,” akasema Bw Skanda.

Bw Skanda alichacha kuwa mbali na kuhamasisha umma kuepuka uchafuzi wa mazingira, vyombo wanavyotengeneza ni vya ubunifu wa hali ya juu kumaanisha fundi husika akiuza vifaa hivyo hujipatia fedha za kujiendeleza maishani.

Mtaalamu huyo anasifu viti wanavyounda kupitia taka za plastiki kuwa bora zaidi kushinda vile vya mbao, plastiki ya kawaida au hata chuma.

“Utapata kiti tunachounda kutokana na taka za plastiki baada ya kupitia awamu mbalimbali mwishowe kinakuwa dhabiti zaidi kushinda hata kile cha mbao za kawaida. Hata bei yake ni ya juu. Utapata kiti cha kawaida cha mbao hapa Lamu kikiuzwa kwa kati ya Sh18,000 na Sh20,000 ilhali hiki cha taka za plastiki tukikiuza kwa Sh30,000 kwenda juu,” akasema Bw Skanda.

Anafichua kuwa utengenezaji wa viti hivyo balozi vya taka za plastiki huchukua muda kwani utalazimika kuzipitisha plastiki kwenye awamu za ukarabati na uboreshaji kabla ya kuanza kuzitumia kutengeneza viti kwa kutumia maarifa asilia.

“Punde tunapokamilisha ukarabati na uboreshaji wa taka hizo za plastiki kwenye karakana yetu, shughuli bayana ya kutengeneza kiti hadi kikamilike huchukua muda usiopungua wiki moja au mbili,” akasema Bw Skanda.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo, hasa walimu na wanafunzi, walisifu Shirika la Flip Flopi, wakitaja kuwa miradi yake inaendana sawasawa na himizo zilizoko kwenye mtaala wa sasa wa masomo wa CBC unaoweka zingatio kwa umilisi.

“Wakati umewadia kwa hawa wabunifu wa Flip Flopi kuanza kujumuishwa sana kwenye masuala ya elimu. Mtaala wa elimu wa CBC unahimiza sana ubunifu, ujuzi au maarifa na kazi bayana. Hapa naona Flip Flopi wafaa kushirikishwa ili kuwapokeza wanafunzi wa CBC maarifa ya kuwafaa maishani,” akasema mwalimu Omar Ali.

Gavana Timamy na Waziri wa Elimu kaunti ya Lamu Sabastian Owanga, kila mara wanapoongoza hafla za mahafali maeneo mbalimbali ya Lamu wamesikika wakitumia sana mfano wa Flip Flopi kuhamasisha na kutilia mkazo wanafunzi kuwa wabunifu ili kujifaidi maishani badala ya kusubiri ajira za kuandikwa afisini punde wanapohitimu masomo au taaluma zao.

Kiti Balozi: Kiti hiki ambacho kimekaliwa na Gavana Issa Timamy kilitengenezwa kwa taka za plastiki na taka nyingine za baharini. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Kalonzo aimarisha mikakati ya kutoshea kwa viatu vya Raila

MAONI: Benny Hinn aliacha nchi hoi badala ya kuiletea...

T L