• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
KMPDU yaahidi kufanya hamasisho wahudumu wa afya wapokee chanjo ya Covid-19

KMPDU yaahidi kufanya hamasisho wahudumu wa afya wapokee chanjo ya Covid-19

Na SAMMY WAWERU

MUUNGANO wa Madaktari, Wataalamu wa Dawa na Madaktari wa Meno (KMPDU) umeahidi kufanya hamasisho kuhakikisha wahudumu wa afya nchini wanapokea chanjo ya Covid-19.

Kaimu Katibu Mkuu wa muungano huo, Dkt Chibanzi Mwachonda amewahimiza wahudumu wa afya kupokea chanjo ya AstraZeneca inayoendelea kutolewa, akisema itawasaidia kuimarisha kinga mwilini.

Amesema wahudumu waliopata chanjo wako katika hali bora, endapo watakumbana na mgonjwa aliyeambukizwa.

Dkt Mwachonda alisema Jumanne KMPDU haitaki kujipata katika njiapanda sawa na iliyopitia mwaka uliopita, 2020, ambapo muungano huo ulipoteza idadi kubwa ya madaktari kufuatia athari za janga la corona.

“Tunawahimiza wahudumu wa afya wapokee chanjo. Hatutaki kushuhudia tuliyokumbana nayo mwaka uliopita,” akasema katibu huyo.

“Itasaidia kukabiliana na magonjwa sugu yanayoambatana na virusi vya corona,” akaelezea.

Dkt Mwachonda alisema KMPDU inaunga mkono utoaji wa chanjo ya AstraZeneca unaoendelea.

Muungano wa wahudumu wa Kimatibabu Nchini (KMA) pia uliahidi kufanya hamasisho kuhusu umuhimu wa upokeaji chanjo.

“Kwa umma na wanasiasa, tunawaomba mzingatie sheria na kanuni zilizowekwa kusaidia kudhibiti msambao zaidi. Vituo vya afya vinapitia nyakati ngumu kutokana na ongezeko la maambukizi,” akasema Katibu Mkuu wa KMA, Dkt Simon Kigondu.

Awali, KMPDU ilikuwa imetilia shaka chanjo inayoendelea kusambazwa, ikilaumu Wizara ya Afya kwa kutoishirikisha.

Aidha, Idara ya Afya imeonya kuhusu ongezeko la visa vya maambukizi ya corona, ikisema hospitali zimejaa wagonjwa.

Taifa kwa sasa linaendelea kukodolewa macho na hatari ya wimbi la tatu la maambukizi ya Covid-19.

You can share this post!

SRC yalenga kupunguza marupurupu ya watumishi wa umma

Hospitali ya rufaa ya KU kushirikiana na Gatundu Level 5